Wapewa ufadhili wa masomo DIT
VIJANA wanawake 10 kutoka vyuo mbalimbali nchini wamepata ufadhili wa masomo ya Shahada ya Uzamili ya Uhandisi wa Nishati Endelevu katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT).
Ufadhili huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa kwanza wa Matumizi Bora ya Nishati wa Tanzania unaosaidiwa na Umoja wa Ulaya (EU) na Programu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP).
Akizungumza leo Dar es Salaam, Makamu Mwakilishii Mkazi wa UNDP Tanzania, Sergio Valdini amesema kuwa wanawake hao vijana wenye vipaji wanawakilisha mustakabali wa usawa wa kijinsia katika nishati endelevu.
“UNDP inayo furaha kushirikiana na DIT kupitia Programu ya Mpango Kazi wa Matumizi Bora ya Nishati unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya kwa kuwapa fadhili wa masomo wanawake vjana 10 siku ya leo,” amesema.
Mbali na kupata ufadhili, mradi huo pia umesaidia DIT katika kuwanunulia vifaa vya matumizi bora ya nishati na maabara mpya ya kisasa ambayo itatumika kwa mafunzo ya vitendo, ushauri, na utafiti katika Usimamizi wa Nishati, Ukaguzi wa Nishati, na Uthibitishaji wa Majengo yaliyokidhi vigezo vya matumizi bora ya nishati.
Ameeleza kuwa mpango huo unalenga kuhakikisha upatikanaji wa nishati nafuu, ya uhakika, endelevu, na ya kisasa kwa watu wote nchini Tanzania.
Kwa upande wake, Mkuu wa Rasilimali Asilia kutoka Unoja wa Ulaya nchini Tanzania, Larnine Diallo, amesema kuwa EU inajivunia kusaidia juhudi za Tanzania za kukuza matumizi bora ya nishati na kuwa na nishati endelevu.
Amesema moja ya hatua muhimu ni kuendeleza vigezo vya kitaaluma na ujuzi katika usimamizi na ukaguzi wa nishati, huku ukiweka kipaumbele kwa wanawake.
“Tumepokea maombi 167 kutoka kwa wanawake vijana kote nchini kwa ajili ya kuomba ufadhili wa masomo. Waombaji walichaguliwa
kutokana na vigezo vyao vya kitaaluma, uwezo wa uongozi, na ahadi zao kuhusu matumizi bora ya nishati,” amesema Diallo.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Bahati Mtono, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Utawala, na Usimamizi, amewataka wanaonufaika na mradi huo kutumia vifaa vya maabara kwa uangalifu pamoja na kutumia maarifa yatakayotolewa.
Pia amewataka kuhakikisha wanakuwa mabalozi kuhamasisha matumizi bora ya nishati, na hivyo, wajitume katika masomo yao.