MOGADISHU, Somalia: WAPIGANAJI 80 wa kundi la wanamgambo wa Al-Shabaab wameuawa katika operesheni za kijeshi na Jeshi la Somalia katika jimbo la Mudug, kamanda mkuu wa jeshi alisema jana.
Wanamgambo hao waliuawa kwenye msitu karibu na mji wa Caad, kulingana na taarifa ya Brig. Jenerali Dayah Abdi Abdulle.
Alisema jeshi, likisaidiwa na vikosi vya ndani, litaendelea na operesheni dhidi ya al-Shabaab.
Matamshi yake yamekuja siku mbili baada ya Wizara ya Ulinzi kutangaza zaidi ya wanamgambo 130 kuuawa katika operesheni Kusini mwa Somalia na kukomboa maeneo makubwa ya ardhi kutoka kwa kundi hilo.
Jeshi hilo likisaidiwa na vikosi vya ndani, limekuwa likifanya operesheni tofauti za kijeshi dhidi ya Al-Shabaab katika mkoa wa kati wa Mudug katika jimbo la Hirshabelle, pamoja na jimbo la Kusini la Jubaland, ambazo zimekuwa zikiendelea tangu mwishoni mwa wiki iliyopita.
Somalia imekuwa ikikabiliwa na ukosefu wa usalama kwa miaka mingi, huku vitisho vikitoka kwa Al-Shabaab na makundi ya kigaidi ya Daesh/ISIS.
Tangu mwaka 2007, Al-Shabaab imekuwa ikipigana na serikali ya Somalia na Misheni ya Mpito ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS), ujumbe wa pande nyingi ulioidhinishwa na Umoja wa Afrika na kuamriwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Kundi hilo la kigaidi limeongeza mashambulizi tangu Rais wa Somalia, ambaye alichaguliwa kwa muhula wa pili mwaka jana, kutangaza vita dhidi ya kundi hilo.
Comments are closed.