WANAMTANDAO wa kupinga rushwa ya ngono Tanzania wenye mashirika jumuishi zaidi ya 150, yanayounda mtandao wa kupambana na rushwa ya ngono wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan asikubali kipendele kinachomhukumu anayedaiwa rushwa.
Akitoa tamko hilo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa mtandao huo, Ruth Meena amesema wanamuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati kipengele hicho kisipitishwe, kwani kinamhukumu mtu aliyetendewa udhalilishaji huo.
Kulingana na mapendekezo ya muundo ya sheria hiyo, kipengele cha 25 (ii) kinaelekeza kumhukumu anayedaiwa rushwa ya ngono.
Profesa Ruth amesema kipengele hicho kitaendelea kuwalinda watu wanaofanya vitendo hivyo na kuwaathiri zaidi wanawake, ambao ndio waathirika wakubwa.
Amesema kipengele hicho kitaongeza ukimya dhidi ya vitendo vya rushwa ya ngono na kusababisha wanawake kuendelea kuathirika bila hatua kuchukuliwa kwa wahusika.
“Tunamuomba Rais Samia na vyombo vyote vinavyohusika na mabadiliko ya sheria hii ikiwa ni pamoja na ofisi ya mwanasheria mkuu, bunge letu tukufu wasikubali pendekezo la kubadilisha kifungu hiki,” alisisitiza.
Naye Mwanamtandao Clement Mwombeki amsema wakati huu kuna ukimya dhidi ya matukio kama sheria itawabana hata watendewa, ukimya utazidi taarifa hazitatolewa na hatua hazitachukuliwa hivyo kutakuwa na taifa linalofumbia macho vitendo vya ajabu.
Akitolea mfano matukio ya baadhi ya taarifa ya rushwa ya ngono, Mwombeki amesema uwepo wa matumizi mabaya ya madaraka katika taasisi za elimu kwa waalimu, wakufunzi na hata viongozi kudai ngono, ili wahusika aidha wapewe stahiki zao au wapendelewe.
“Uwepo wa matumizi mabaya ya madaraka katika huduma za afya mathalani, vyombo vya habari vilitujuza jinsi mama mmoja aliyelazimishwa kutoa rushwa ya ngono, ili mtoto wake mahututi apatiwe huduma.
“Kiongozi mmoja wa dini alitoa ushuhuda kuhusu Profesa mmoja aliyekiri kwake kusababisha wanafunzi wengi aidha kufeli na wengine kujiua kwa kukataa kutoa rushwa ya ngono,” amesema.
Amesema pia, uwepo wa matumizi mabaya ya madaraka katika maeneo ya kazi mfano, kuna dada aliyefukuzwa kazi kwa ajili ya uthubutu wa kukataa rushwa ya ngono, ambapo ilimchukua takribani miaka nane kushinda kesi yake mahakamani, na hata baada ya ushindi ilimchukua miaka miwili kupatiwa stahiki zake.