Wapinzani wa Yanga vitani leo

PRETORIA, Afrika Kusini: SIKU tatu kabla ya kurudiana na Yanga SC katika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL), Mamelodi Sundowns leo majira ya saa 02:30 usiku, watakuwa wenyeji wa vibonde Richards Bay katika michezo ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL), Uwanja wa Loftus Versfeld, jijini Pretoria.

Katika msimamo wa PSL, Mamelodi ni kinara wa msimamo akikusanya alama 46 katika michezo 18 huku wapinzani wao Richards Bay wakiwa nafasi ya 15, nafasi moja kutoka chini ya msimamo. Wamevuna jumla ya alama 14 katika michezo 21.

Katika michezo mitano waliyokutana katika mashindano tofauti, Mamelodi ameshinda mechi zote wakiwa na jumla ya magoli 11 ya kushinda na kuruhusu mabao mawili pekee.

Advertisement

Wawakilishi wa Tanzania, Yanga SC wapo angani muda huu kuelekea Afrika Kusini kukabiliana na Mamelodi Aprili 05 Ijumaa hii katika Uwanja wa Loftus Versfeld baada ya suluhu tasa 0-0 katika mchezo wa awali Machi 30, 2024, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Hii inaweza kuwa nafasi kwa Yanga SC kuwasoma kwa karibu wapinzani wao wakiwa nyumbani, kutazama hamasa ya mashabiki, hali ya hewa na joto la mchezo wa ugenini siku za usoni.