Wapinzani waisifu serikali marekebisho tozo

Katibu Mkuu wa chama cha ADC, Doyo Hassan Doyo

VIONGOZI wa vyama vya siasa nchini wameipongeza serikali kurekebisha tozo na wameshauri itafute vyanzo vingine kuongeza mapato.

Katibu Mkuu wa chama cha ADC, Doyo Hassan Doyo alisema tozo si tatizo kwa sababu malengo yake yalilenga maslahi ya Watanzania, lakini ilitakiwa kwanza kuwepo na ushirikishwaji wa wadau na elimu kutolewa kwa wananchi.

“Shida ilianza pale wananchi walipoanza kukatwa fedha nyingi tena double, ukitoa benki unakatwa, ikiingia kwenye simu na ukiitoa unakatwa na mshahara wenyewe pia unakatwa kodi. Ni hatua nzuri serikali kuliona hili na kulifanyia kazi,” alisema Doyo.

Advertisement

Aliongeza: “Ndio maana nasema tozo hii isifutwe moja kwa moja bali ipunguzwe sana ili wananchi wasipate uchungu.”

“Jana (juzi) nilitoa shilingi 400,000 benki nimekatwa shilingi 20,000, hii inauma sana. Lakini kama ningekatwa shilingi 1,500 au 2,000 kuna shida gani kama ni kwa maendeleo ya nchi yangu?”

Aliyewahi kuwa Mgombea Urais kupitia Chama cha Demokrasia Makini, Cecilia Mmanga alishauri serikali kuangalia njia mbadala ya kutafuta mapato kupitia kodi badala ya kuwabana Watanzania kupitia tozo.

Mmanga alisema yapo maeneo mengi yanayoweza kuwekewa kodi au tozo na kuingiza fedha kuliko eneo hilo la miamala ya kielektroniki linalowagusa watu wanaokatwa kodi kila siku.

Alitaja maeneo yanayoweza kuisaidia serikali kuingiza mapato zaidi kuwa ni michezo, michezo ya bahati nasibu, kubeti, kodi za magari, leseni za barabarani na bima.

Mwenyekiti wa Taifa wa DP, Philipo Kumbo alisema suala la hilo la tozo ni shirikishi hivyo serikali inao wajibu wa kuendelea kupata maoni ili kuboresha zaidi.

“Mimi niligombea mwaka 2020 Urais niko na wenzangu kama 15 hivi. Urais ni kiti kimoja, wote 15 hatuwezi kukalia hizo, lakini tulipigiwa kura japo chache na baadhi ya wananchi, basi na sisi tutumike kwenye masuala kama haya ya maendeleo kutoa maoni yetu kwa maslahi ya Taifa,” alisema Kumbo.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alitangaza bungeni marekebisho yaliyofanywa kwenye tozo kwa kufuta ya kuhamisha fedha kutoka benki kwenda mitandao ya simu, kufuta tozo ya kuhamisha fedha ndani ya benki moja na kufuta tozo ya kuhamisha fedha kutoka benki moja kwenda benki nyingine.

Aidha, juzi Kamishna Msaidizi wa Uchambuzi wa Sera wa Wizara ya Fedha na Mipango, William Mhoja alibainisha kuwa serikali inaendelea kupokea ushauri na maoni kuhusu tozo baada ya uamuzi wa kufuta na kupunguza baadhi uliotolewa bungeni juzi.