VIONGOZI na wanasiasa wa vyama vya upinzani wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kubadili muundo wa wizara mbili na kuunda wizara mpya ya Mipango na Uwekezaji.
Rais Samia juzi alimteua Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji.
Pia aliunda Wizara ya Fedha na akamteua Dk Mwigulu Nchemba aiongoze wizara hiyo. Awali Dk Mwigulu alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango.
Aidha, Rais Samia ameunda Wizara ya Viwanda na Biashara na itaongozwa na Dk Ashatu Kijaji aliyekuwa Waziri wa iliyokuwa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Kabwe Zitto alisema mabadiliko hayo yataboresha uratibu wa shughuli za uchumi wa nchi.
“Nimefurahi Tume ya Mipango imerudi, tulifanya kosa kubwa kuifuta…nawatakia kila la kheri wote walioteuliwa,” alisema Zitto.
Katibu Msaidizi wa Chama cha Wananchi (CUF) Tanzania Bara, Magdalena Sakaya alisema mabadiliko yamefanyika kwa wakati mwafaka kwani nchi ilikosa mipango.
Alimpongeza Rais Samia kwa uamuzi huo na kusema mara zote amekuwa makini na hasiti kufanya mabadiliko anapoona kuna mahali panastahili.
“Mimi nimeangalia katika awamu zote, awamu hii inafanya mabadiliko ya mara kwa mara mara nyingi, hii unajua maana yake nini? Rais anafuatilia na anataka kazi ifanyike vizuri kwa hiyo akiona kuna mahali kuna jambo linalega hasiti kufanya mabadiliko, na kwenye hilo huwa hatizami urafiki, sura wala rangi ya mtu,” alisema Sakaya, mbunge wa zamani.
Alisema kwa kuitenga Wizara ya Mipango na Uwekezaji peke yake, nchi itarajie kukuza uchumi endapo walioteuliwa kuiongoza watafahamu anachokitaka Rais Samia.
“Tume ya Mipango iliporejeshwa nilifurahi kumbe ile ilikuwa moja, namba mbili Rais ameweka Wizara ya Mipango na Uwekezaji peke yake, pongezi sana kwake wawekezaji lazima wawepo maana huwezi kujenga nchi peke yako,” alisema Sakaya.
Alimpongeza Profesa Kitila akisema kazi yake nzuri aliyofanya alikopita inafahamika hivyo ana imani atafanya vizuri.
Profesa Kitila aliwahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uwekezaji) katika Serikali ya Awamu ya Tano kuanzia mwaka 2020 hadi Aprili 2021 alipoteuliwa na Rais Samia kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara alikohudumu hadi Januari mwaka jana.
Aidha, Sakaya ametoa ushauri kwa Tume ya Mipango itazame changamoto zilizopo na kutafuta suluhisho.
Katibu Mkuu wa Chama cha ADC, Hassan Doyo alisema mabadiliko hayo ni mazuri kwani kwenye watu lazima kuwe na mipango.
“Vipaumbele vyao iwe kwenye maisha ya watu ya kila siku, miundombinu, afya, maji,” alisema Doyo.
Mhadhiri wa Chuo cha Kikatoliki Mbeya, Samson Mwigamba alipongeza na kutaka wizara ibuni kodi mpya kwa ajili ya ustawi wa uchumi.
Tume ya Mipango
Tume ya Mipango ilifutwa mwaka 2018 kwa kuiunganisha na Wizara ya Fedha. Juni 28, 2018, Kamati ya Bunge ya Bajeti ilishauri serikali kutoifuta sheria iliyoanzisha tume hiyo kwa kusema ina tija kwa taifa.
Hivi karibuni, Bunge lilipitisha Muswada wa Kuanzisha Sheria ya Tume ya Mipango ya Mwaka 2023 itakayotumika Tanzania Bara.
Tume hiyo itakuwa chini ya Uenyekiti wa Rais wa Tanzania na pia itakuwa chini ya idara inayojitegemea chini ya Ofisi ya Rais.
Sheria hiyo imeeleza kuwa tume hiyo itakuwa na wajibu wa kusimamia uchumi, mchakato wa upangaji na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya taifa kama ilivyoidhinishwa kwa lengo la kuhakikisha kuwa kunakuwa na ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa na maendeleo kama ilivyokusudiwa katika mfumo husika.
Comments are closed.