Wapinzani wamsifu Samia ujio wa Kamala

VYAMA vya siasa nchini vimesema Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris anakuja kufanya ziara nchini kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameimarisha demokrasia na diplomasia.

Harris anawasili nchini leo kwa ziara barani Afrika akitokea Ghana na anatarajiwa kwenda Zambia.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mrema akizungumzia ziara hiyo alisema huo ni mwendelezo wa ziara za viongozi wakubwa duniani.

“Hii inaonesha diplomasia yetu inazidi kuimarika, baada ya hatua kuchukuliwa na serikali hapa nchini, sasa wameonesha nia wanaanza kuja.

“Lakini pia Rais Samia anashiriki vikao vya Umoja wa Mataifa, amefungua milango na viongozi wanakuja, kwa sababu hata sisi tulienda,” alisema Mrema.

Akizungumzia manufaa ya ziara hii kiuchumi, Mrema alisema ujio wake ni muhimu kwa taifa kwani vyombo vyote vya dunia vitatumika kwa siku hizo tatu kumulika ziara hiyo hivyo ni suala la viongozi na taasisi wawe wamejipanga kuinadi nchi.

“Msafara huu tukiutumia vizuri tutajitangaza sana duniani, tuangalie sisi tunataka dunia ione nini, tuchague vichache tuvinadi vizuri. Je, tunauza nini, kama ni utalii je, tunatangaza vivutio gani, kama ni madini, tunatangaza aina gani, tanzanite au dhahabu? Ni suala la kujipanga na huenda taasisi zetu zimeshafanya hayo,” alisema Mrema.

Akizungumzia kuimarika kwa mahusiano, Mrema alisema hadi sasa uhusiano unaonesha uko vizuri ndio maana wanakuja na kuwa ni vyema kama nchi ikaendelea kuimarisha zaidi ili mataifa mengine yaje.

Mkurugenzi wa Habari, Uenezi, Mahusiano na Umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Mohamed Ngulangwa alisema ziara ya Kamala ina tafsiri nyingi, lakini mojawapo ni kufunguliwa kwa diplomasia na kuimarika kwa demokrasia nchini.

“Muda mrefu tumeona hata watangulizi wa Kamala walifanya ziara Tanzania, ingawa hatuwezi kufahamu kwa undani wana maslahi yao, ila tafsiri mojawapo ni nchi imefunguliwa kidiplomasia na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema Ngulangwa.

Alisema Rais Samia ametumia muda wake kwenda nje ya nchi kuimarisha kidiplomasia na pia ameitangaza nchi kiutalii kupitia filamu ya The Royal Tour.

“Tutarajie nchi kufunguka zaidi kiuchumi kwa sababu ujio wa kiongozi huyo unatazamwa na dunia, ni fursa kwa sisi pia kutangaza nchi kupitia ziara hii,” alisema Ngulangwa.

Alisema pia katika ziara hii nchi itarajie kuimarika na kukua kwa diplomasia ya uchumi kwa sababu mazingira ya biashara, uwekezaji yanaendelea kuboreshwa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia Makini, Ameir Hassan Ameir alisema viongozi wa mataifa makubwa kuitembelea nchi inaonesha namna Rais Samia anavyoiongoza nchi kidemokrasia.

“Rais Samia anavyoendesha nchi kuna uhuru kwa vyama vya siasa, hakuna chama kinapiga kelele sasa, uchumi wa nchi unapanda, hata mataifa ya nje yameridhishwa na demokrasia na utawala nchini,” alisema Ameir.

 

Habari Zifananazo

Back to top button