Wapongeza kuanzishwa kwa Mfuko wa Hijja

KUANZISHWA kwa Mfuko wa Hijja kumetajwa kuwa kutaongeza nafasi nyingi zaidi kwa waumini wa dini ya Kiislamu kutekeleza ibada ya hijja Makka, nchini Saudi Arabia.

Baadhi ya wananchi waliohojiwa wakiwamo viongozi wa dini ya Kiislamu, walisema hiyo ndiyo njia mwafaka kwa watu wenye nia ya kufanya ibada hiyo ambapo mfuko utabuni njia ya kuwasaidia ikiwemo kuwakopesha.

Imamu wa Msikiti wa Donge Unguja, Juma Himidi (47) alisema ibada hiyo inatakiwa kutekelezwa kwa waumini wenye nguvu kwa sababu yapo matukio mengi yanayohitaji mbinu na maarifa kuyatekeleza.

Alisema katika ibada ya kurusha mawe kwa ajili ya kumpiga shetani inahitajika nguvu kwa sababu katika kipindi hicho zinakuwepo harakati nyingi na msongamano mkubwa wa waumini.

”Tunazipongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuanzisha Mfuko wa Hijja ambapo matarajio yetu makubwa watu wengi watapata nafasi ya kwenda kuhiji ambapo mfuko utakuwa na utaratibu wa kuwaunga mkono watu wenye nia,” alisema.

Imamu wa Msikiti wa Makunduchi Wilaya ya Kati Unguja, Abdallah Hussein Pandu alisema kuanzishwa kwa mfuko huo kutawawezesha Waislamu wengi kwenda kufanya ibada ya Hijja ukichukulia ukweli kwamba ibada hiyo inahitaji kiwango kikubwa cha fedha.

Alisema wapo viongozi wengi wa dini hawajapata fursa ya kuhiji Makka huku wengi wao wakipindukia umri wa miaka 70 ambao hawana nguvu za kutekeleza ibada hiyo kikamilifu.

”Ukiwa mtu mwenye umri wa miaka 70, uwezo wa kutekeleza ibada ya hijja ni mdogo unakuwa kama mgeni mwalikwa…ibada ya hijja inahitaji nguvu za ziada kukamilisha vitendo vyote muhimu na hapo ndipo hijja yako inapokamilika,” alisema.

Ofisa mstaafu kutoka katika Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana, Assa Kheri alisema gharama za Ibada ya Hijja zimeongezeka na inakuwa vigumu kwa Waislamu wengi wenye nia kutekeleza ibada hiyo.

Alisema ili kutekeleza ibada hiyo, inatakiwa kuwa na Sh milioni 14 ikiwa ni gharama zote za kutekeleza ibada hiyo ambazo fedha hizo kwa Waislamu wengi wa kawaida ni nyingi.

Kwa upande wake, Sauda Hijja Faki anaunga mkono kuanzishwa kwa Mfuko wa Hijja akisema: “Hatujachelewa…wenzetu kama nchi za Malaysia na Indonesia raia wake hutekeleza ibada ya hijja wakiwa na umri wa miaka 30 hadi 40…sisi tunakwenda hijja tukiwa tayari wengi wao wastaafu tumechoka.”

Katibu Mtendaji wa Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar, Shehe Abdallah Talib Abdallah alisema mchakato wa kuanzishwa kwa mfuko huo zimekamilika na utakwenda sambamba na maboresho makubwa ya taasisi hiyo.

Alisema katika maboresho hayo sasa yataifanya Taasisi ya Wakfu na Mali ya Amana kuwa inayojitegemea huku ikifanya shughuli zake katika sura ya kibiashara zaidi ikiwemo kujenga majengo na kuyakodisha kwa watu binafsi.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema ipo katika hatua za mwisho za kuanzishwa kwa Mfuko wa Hijja ambao utawawezesha wananchi wengi kwenda kutekeleza ibada.

Habari Zifananazo

Back to top button