Wapongeza mradi wa maji Mtwara

WAKAZI wa mtaa wa Mangamba ‘Airport’ , uliopo Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara, wameishukuru serikali kwa kuwapelekea mradi wa maji unaogharimu zaidi ya Sh mil. 500.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti leo Aprili 2, 2023 wakati Mwenge wa Uhuru ulivyotembelea maeneo hayo, baadhi ya wananchi hao wamesema mradi huo wa ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa lita 500,000 utawanufaisha sana ukikamilika.

‘’Sisi wakazi wa Mangamba kupitia mradi huu ni matumaini yetu tutaondokana na changamoto ya uhaba wa maji, “ anasema Zainab Said na kuongeza:

“Tunaishukuru sana Serikali yetu kwa kutuletea maji haya ambayo yataenda kumaliza chagamoto yetu,’’amesema Zainabu.

Naye Somoe Likundasi  amesema, kitendo cha serikali  kuwapelekea mradi huo ni kitamaliza kero ya maji kwa wakazi wa maeneo hayo, lakini pia maeneo jirani kwa sababu mradi unapowekwa unanufaisha sehemu kubwa ya wananchi na siyo eneo la mradi pekee.

Akisoma taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mtwara Mjini  (MTUWASA), Mhandisi Rejea Ng’ondya, amesema lengo la mradi ni kuongeza huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa manispaa hiyo kwani tanki linalohudumia sasa lina ujazo wa lita 90,000.

Akiweka jiwe la msingi  katika mradi huo wa maji, kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Abdalla Shaib Kaim, amemtaka mkandarasi anayejenga mradi huo kufanya kazi ndani ya mkataba, ili wananchi wapate huduma hiyo ya maji kwa wakati.

Amepongeza mradi huo kutokana umekidhi vigezo na ubora,  akisema kuwa serikali ina dhamira ya dhati kuwajengea miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao ukiwemo huo wa maji.

Ujenzi wa mradi huo ulisainiwa Septemba mwaka 2022 na mkandarasi alianza kufanya kazi Desemba, 2022 na unatarajiwa kukamilika Mei, 2023.

Habari Zifananazo

Back to top button