Wapongeza mradi wa maji Mushabaiguru
WAKAZI wa Kijiji Mushabaiguru, Kata Kihanga wilayani Karagwe, wameipongeza serikali kwa kuhakikisha inarejesha amani katika familia zao baada ya mradi wa maji wa Ishabaiguru kukamilika na kusogeza huduma kwao na wengine kuunganisha maji nyumbani kwao.
Wananchi ambao waliokusanyika kumpokea Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nadhifa Kemikimba alipotembelea kijijini hapo mwishoni mwa wiki,kukagua mradi huo, walisema upatikanaji wa maji Kata ya Kihanga unapaswa kutunzwa katika vitabu na kuwekwa kumbukumbu za vizazi vijavyo.
Akizungumza mkazi wa kijiji hicho, Evodia Edward amesema kwa sasa Familia zimerejesha utulivu na amani, kwani kulikuwa na upotevu wa saa 3 hadi 4 kufuata maji, ambayo pia yalikuwa machafu
.
“Lakini kwa sasa tunatumia dakika 3 kuchota maji na wengine tumeweka majumbani hakuna ugomvi tena kwa wanaume zetu, wala mateso kwa watoto wetu,” amesema.
“Changamoto ya kuondoa amani katika familia zetu ilikuwa ni muda mrefu unaotumika kufuata maji Kihanga, utekelezaji wa mradi wa Ishabaiguru sio Furaha tu kwa wanawake, bali wanaume na watoto wetu, kwani ugomvi ndani ya familia hautakuwepo tena.
“Hakuna anayetumia dakika 10 kufuata maji tunapata maji ndani ya dakika 3 hadi 5 ni kicheko na furaha kwetu, “alisema mwanachi mwingine Seperansia Paschale kwenye mkutano huo.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu huyo aliwaambia wananchi kuwa lengo la serikali ni kuboresha maisha yao kwa kuwapatia maji safi karibu na nyumbani na maji hayo kusogezwa katika taasisi zao za umma kama hospital, shule, zahanati na kila sehemu.
“Kilio chenu kikubwa ilikuwa ni umbali mrefu wa kufuata maji, kilio kingine ilikuwa ni kwenda hospital na ndoo za maji kuwahudumia wagonjwa, shule zenu watoto kukosa kunywa uji kwa ukosefu wa maji.
“Niwaondolee wasiwasi zaidi na muendelee kuwa na amani pamoja na kutunza miundombinu ya maji, serikali ipo kazini na inachapa kazi kazi, “alisema Kemikimba.
Mhandisi wa maji kutoka Ruwasa wilaya ya Karagwe, Justo Mutabuzi alisema kuwa mradi huo umetekelezwa na mkandarasi Buzubona & Sons na kusimamiwa na Ruwasa kwa gharama ya shilingi Milioni 497, ambapo wananchi wapatao 1,715 katika Kijiji Cha Mushabaiguru watanufaika na maji safi na salama.