Wapongeza Sh bilioni 3.5 kutumika uzalishaji vifaranga vya samaki

KINGOLWIRA, Morogoro: KAMATI ya kudumu ya Bunge ya Utawala , Katiba na Sheria imeipongeza Serikali kwa kutoa fedha zaidi ya Sh bilioni 3.5 kwa ajili ya kupanua uwekezaji katika Kituo cha Kuendeleza Ukuzaji  Viumbe Maji Kingolwira  mkoani Morogoro ili kiongeze  uzalishaji wa vifaranga vya samaki hadi kufikia milioni moja kwa mwezi kutoka vifaranga 100,000.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Florent Kyombo ametoa pongezi hizo wakati kamati hiyo ya kudumu ya bunge ilipotembelea kwenye kituo hicho kilichopo katika Manispaa ya Morogoro.

Kyombo ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mbunge wa Jimbo la Nkenge amesema   Serikali ya awamu ya sita chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewezesha na kufanikisha uwekezaji huo mkubwa.

Advertisement

“Tunaipongeza Serikali kwa uwekezaji huu wa Sh bilioni 3.5 zinazotolewa kwa awamu kwa ajili ya mradi wa uzalishaji wa vifaranga vya samaki ambavyo inasambazwa nchini kote ili wananchi kupata lishe na kukuza Uchumi,” amesema Kyombo.

“Sisi tumeliona hili ni jambo jema na umeona kwa macho nah ii ni fursa ya kushauri zaidi kupitia serikali yetu ili kupata kitu chenye thamani kulingana na fedha zilizowekezwa” amesisitiza Kyombo.

Kwa niaba ya Kamati hiyo amekipongeza  kituo hicho  kwa kuanza kuzalisha chakula cha samaki ambao ni mradi unaoweza kusaidia kuokoa fedha zilizokuwa zinatumika  kununulia chakula kutoka nje .

“Kamati yetu imeridhishwa na hatua hii  ya mwanzo na kwamba mradi huu  na mingine iliyopo kwenye  mikoa tofauti itakapokamilika itakuwa ni yenye  wenye thamani kubwa kwa wananchi wetu kijamii  hasa lishe , kiuchumi na kwa Taifa kiujumla” amesema  Kyombo.