Wapongeza sheria kulinda taarifa binafsi

VIONGOZI wa vyama vya siasa na wananchi wameipongeza serikali kuwasilisha bungeni na bunge kupitisha Muswada wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

Katibu Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu alisema wanaunga mkono kuwepo kwa sheria hiyo ili kulinda taarifa binafsi za watu.

“Rai yetu ni ni muhimu kuweka uwiano kwa ajili ya usalama wa taarifa za ulinzi na usalama wa taifa  letu zilindwe lakini pia kuwepo na uhuru wa kupata habari zenye maslahi kwa umma,”alisema Shaibu.

Kiongozi wa chama cha NCCR-Mageuzi, Joseph Selasini alisema sheria hiyo italinda faragha za watu kwa sababu wapo walioharibiwa au kupoteza uaminifu kwa kusambazwa habari zisizo na ukweli.

“Ninaunga mkono hiyo sheria kila mtu ana haki na faragha, watu wengi wamechafuliwa na familia zimeparaganyika imefikia hata wengine wamekufa kwa presha, kwa sababu ya chuki mtu anamua kusambaza vitu vya kifaraga kwenye mitandao kumchafua mwingine,”alisema Selasini.

Alisema sheria hiyo itakuwa suluhu kwa kuwa hata kwenye taasisi  wapo viongozi faragha zao zimewekwa hadharani na kuwaharibia sifa na hivyo kukosa kuamiwa tena.

Selasini alisema unahitajika umakini katika kuitekeleza sheria hiyo ili kusiwe na vikwazo vya kupata habari kwa umma kwa kisingizio cha sheria ya sheria hiyo.

“Uhuru wa mtu kupata habari za umma unabaki pale pale lakini pia uhuru na faraga ya taarifa binafsi lazima vilindwe,”alisema Selasini.

Mdau wa habari nchini, Kajubi Mukajanga alisema  ni  hatua nzuri na kuwa sheria hiyo ilipaswa iwe imeshaanza kutumika kwani mitandao nchini imetumika kwa njia moja  kuharibu maisha ya watu wengi.

“Athari za mitandao ni kubwa, sheria hii ni nzuri na sisi tunapongeza hatua hii ya serikali kuipeleka ingawa pia imechelewa lakini enzi hizi za mitandao duniani kote imetumika kwa njia moja kuharibu maisha binafsi ya watu na kazi zao,”alisema Mukajanga.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Sera wa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo visivyo vya Serikali Tanzania (Tamangsco), Benjamin Nkonya alisema sheria ni muhimu ili kuepusha mijadala ya faragha za watu mitandaoni.

“Hii sheria itasaidia masuala binafsi ya faraga yasiwepo tena mitandaoni, mambo ya umma ndiyo yawekwe yajadiliwe, ila sio faraga za watu, haya mambo yalileta shida kwenye familia,”alisema Nkonya na akasema sheria hiyo isitumike kulinda uovu.

Bunge lilipitisha Muswada wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya Mwaka 2022 ambayo inaweka masharti ya misingi ya ulinzi wa taarifa hizo.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x