Wapongeza TASAF kwa kutekeleza miradi ya elimu

Wapongeza TASAF kwa kutekeleza miradi ya elimu

WANANCHI wa Kijiji cha Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja wameupongeza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa kutekeleza miradi ya elimu ikiwemo ukumbi wa matayarisho ya mitihani kwa wanafunzi.

Mkazi wa Kizimkazi Dimbani, Mwanaidi Juma alisema kwa muda mrefu wanafunzi wa shule katika eneo hilo walikuwa wakikabiliwa na ukosefu wa ukumbi wa kufanya mitihani ikiwemo ya majaribio na taifa.

Alisema mradi wa ujenzi wa ukumbi wa mitihani kwa wanafunzi ni matokeo ya ubunifu wa wananchi hao walioibua mradi huo ili kuondoa usumbufu wa watoto wao.

Advertisement

”Tunaupongeza mradi wa ujenzi wa ukumbi wa mitihani katika shule ya Dimbani Kizimkazi ambao kwa kiasi kikubwa utaongeza ufanisi wa wanafunzi wetu na kuongeza ufaulu wa mitihani ya taifa,” alisema.

Aidha, Dadi Faki ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Tasaf ya wilaya alisema mradi huo ni matokeo ya kilio kikubwa cha wananchi ambapo kabla ya hapo wanafunzi walikuwa wakipata usumbufu wa kuhangaika kutokana na ukosefu wa ukumbi wa aina hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja, Rajab Mkasaba alisema ufunguzi wa ukumbi wa wanafunzi kufanya mitihani kwa kiasi kikubwa utaongeza ufanisi wa wanafunzi kupata mafanikio makubwa ikiwemo ufaulu wa mitihani ya taifa.

Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Muhamed Mussa alisema kukamilika kwa ukumbi wa wanafunzi kufanya mitihani kwa kiasi kikubwa utapunguza msongamano wa wanafunzi wakati wanapofanya mitihani ya majaribio na taifa.

”Mikakati ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuona kwamba zinakuwepo kumbi zaidi katika shule kwa ajili ya kufanya mitihani wanafunzi wake zenye nafasi ya kutosha,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Dk Ladislaus Mwamanga alisema ujenzi wa ukumbi huo ni sehemu ya mikakati ya Tasaf kuona changamoto zinazowakabili wananchi ikiwemo wanafunzi zinapata majibu yake haraka.

Alisema mradi huo umeibuliwa na wananchi wenyewe baada ya kuona umuhimu na changamoto zilizokuwepo awali za tatizo la ukosefu wa ukumbi wa wanafunzi kufanya mitihani yao.

”Matarajio yetu makubwa kuona ukumbi huu utaongeza ufanisi wa wanafunzi katika ufaulu wa mitihani ya majaribio na taifa hatua ambayo itaongeza wahitimu,” alisema.

Jengo la ukumbi wa mitihani katika Shule ya Kizimkazi Dimbani lilifunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kugharimu Sh milioni 120 ukiwa na uwezo wa wanafunzi 300 kufanya mitihani kwa wakati mmoja.

 

 

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *