Wapongeza uanzishwaji sekondari ya Nyabange  

Sekondari Nyabange kuitwa Sagini 

WAZAZI wa wanafunzi wanaosoma katika sekondari ya Kemoramba, ambao wanaishi Kijiji cha Nyabange, Kata ya Nyankanga mkoani Mara, wameeleza madhira yanayowapata watoto hao na kwamba yatakomeshwa na ujenzi wa Sekondari ya Nyabange.

Awali ilielezwa na Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Husna Juma kuwa serikali imepeleka Sh milioni 40 kwa ajili ya kuanzisha ujenzi wa sekondari hiyo, ili watakaofaulu darasa la saba mwaka huu, waanze kidato cha kwanza kwenye shule hiyo, Januari mwakani.

Diwani wa Kata hiyo, Jackob Shasha alisema wanafunzi hao wanatembea kati ya kilometa 16 hadi 20, kwenda na kurudi shuleni, hali inayowaathiri kwa namna na viwango tofauti.

Advertisement

“Wadhibiti ubora wa elimu walitutembelea shuleni Kemoramba, wakakokotoa umbali unaotembewa na watoto wanaotoka kijiji hiki, wakiwemo wa kidato cha kwanza ambao kiumri ni wadogo, wakasema haifai,” alisema Shasha.

Ikiwa mtoto anatembea kilometa 20 kwenda na kurudi shuleni kwa kutwa, inamaanisha kwa siku tano anatembea Km 100 huku kwa siku 20 anazokwenda shuleni katika mwezi mmoja (J.tatu – Ijumaa × wiki 4) anatembea umbali wa Km 400 sawa na Km 1, 200 kwa miezi mitatu.

Mkazi wa Kijiji cha Nyabange, Misori Matiku alisema kutokana na umbali huo ,wanafunzi wengi wamekuwa wakiomba msaada kwa wenye vyombo tofauti vya usafiri (lift), lakini baadhi ya watu hao wamekuwa wakiwatendea ukatili na baadhi kusababishiwa mimba za utotoni na maradhi.

“Pia kuna wanaopata ajali, mfano mwaka huu tumelifiwa na watoto wawili hapa kijijini waliogongwa na magari wakienda na kurudi shuleni, mimba ndiyo usiseme yaani tunashukuru sana ujenzi wa sekondari yetu,” alisema Matiku.

Alisema hivi karibuni binti mwingine (majina yanahifadhiwa) alinusurika kubakwa na mwendesha bodaboda, aliyekuwa amemsaidia usafiri, lakini badala ya kumfikisha alikotakuwa kumshusha, akamuingiza vichakani kwa lengo la kumbaka, lakini kelele za binti zilizosababisha wanakijiji kumnusuru, ingawa mwanaume alitoroka.

Naye Wambura Mbunduki, alisema wanafunzi wengi wanaomaliza darasa la saba katika Shule ya Msingi Nyabange, wanafaulu kwa alama za juu, lakini wanapomaliza kidato cha nne kwenye Sekondari ya Kemoramba wengi hawafaulu kutokana na changamoto nyingi wanazokabiliana nazo, wakienda na kurudi kutoka shuleni.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Agostino Simon, alisema baada ya Mkutano Mkuu wa Kijiji hicho, waliafikiana kila kaya ichangie Sh 4,000 kwa ajili ya kuchangia ujenzi huo, ambapo wanatakiwa kununua mchanga, kokoto, mawe na kwamba ujenzi utaanza wakati wowote kuanzia sasa, ikitarajiwa kukamilika ndani ya Siku 30.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *