WANANCHI wa Wilaya Karagwe mkoani Kagera wameondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando iliyopo jijini Mwanza, baada ya serikali kukamilisha ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi na kufungwa vifaa tiba vya kisasa katika hospitali hiyo.
Baadhi ya wananchi ambao wamekutana na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatuma Mwasa wamesema wanaridhishwa na huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo na hakuna wasiwasi, ukilinganisha na miaka ya nyuma, ambapo walilazimika kufuata huduma nyingi katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando iliyopo Mwanza.
“Kipindi cha nyuma changamoto kubwa ilikuwa ni kupata huduma nzuri za afya , kwa sasa serikali yetu imerahisisha huduma zote za upasuaji, hakuna tofauti tena kati ya Bugando na Karagwe.
“Kkwa ujumla wananchi tunaridhishwa na huduma zote zinazotolewa , changamoto ndogondogo za uwepo wa watumishi tunaamini serikali itazitatua ,”amesema mwananchi Frank Frederick kwa niaba ya wenzake.
Katibu wa Hospitali ya Wilaya ya Karagwe, Samson Hingi amesema ujenzi wa hospitali hiyo ulianza mwaka 2019 na kwa sasa huduma nyingi zinapatikana hospitalini hapo, hivyo gharama za wananchi kupewa rufaa na kufuata huduma za afya mbali zimepungua.
Amesema kuwa mpaka sasa gharama za ujenzi wa hospitali hiyo Sh bilioni 3.5 na asilimia 60 ya vifaa tiba vya kisasa vimefungwa katika vyumba vya Hospitali na wagonjwa wanapata huduma nzuri.
“Changamoto kubwa iliyobaki ni majengo ya nyumba za watumishi , wengi wanaotoa huduma hapa kwa wagonjwa wanatoka nje ya eneo hili kwa zaidi ya kilometa 7, hivyo ikitokea tukapata wagonjwa wengi ni mtihani.
“Katika hospitali hii kwani hakuna majengo ya kupangisha, bado eneo ni jipya, changamoto nyingine inawapata wagonjwa na wananchi wanaotakiwa kupata huduma za hapa kukosa daladala kutoka Kayanga mjini hadi Hospital ya Wilaya,”amesema Hingi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatuma Mwasa, ameridhishwa na utendaji kazi pamoja na ukamilishaji majengo ya kutolea huduma katika hospitali hiyo na kutoa wito kwa watumishi wa afya kuendelea kuwahudumia wananchi kwa moyo mmoja.
“Nawapongeza kwa usimamizi mzuri pamoja na usafi wa mazingira ya hospitali nzima, ikiwemo utunzaji wa miundombinu , hospital nyingi ukitembelea unakuta mazingira hayaridhishi, “ amesema Mwasa.
Amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na Mkuu wa Wilaya ya Karagwe kuhakikisha wanaweka mpango wa kupatikana magari madogo ya abiria, ambayo yataweka gharama ndogo kwa wananchi wanaoenda kupata huduma
Comments are closed.