WAKAZI 1, 000 wa Kijiji cha Mkomo, Kata ya Chawi, Halmashauri ya Mji Nanyamba Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara watanufaika na mradi wa ujenzi wa zahanati unaogharimu zaidi ya Sh milioni 74.
Akizungumza leo katika ziara ya ukaguzi wa mradi huo uliofanywa na Mwenge wa Uhuru na kuweka Jiwe la Msingi, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Dadi Salumu amesema uwepo wa mradi huo ni faida kubwa kwa wananchi wa kijiji hicho, kwani utawapunguzia adha ya kutembea kilometa tano kufuata huhuma ya afya kijiji jirani cha Chawi.
“Leo tunavyopata zahanati kijijini kwetu tunashukuru, tunajua adha itapungua ya kwenda mbali kufata huduma hii, ni faida kubwa kwetu kwa sababu usiku na mchana saa 24 tutapata huduma, ni jambo la kushukuru hatukuwa na zahanati kabisa kijini kwetu, “ amesema.
Amesema awali kabla ya uwepo wa zahanati hiyo, wanakijiji hasa wajawazito walikuwa na changamoto ya kutembea umbali mrefu kwa kutumia usafiri wa pikipiki, ili kuwahi huduma ya afya na endapo usafiri huo ukikosekana wanalazimika kutumia baiskeli, hali ambayo inaleta usumbufu kwa akina mama hao.
Sofia Salumu mkazi wa Kijiji hicho amesema: “Sisi akina mama tulikuwa tunapata shida sana unapofika wakati wa kutaka kujifungua kwa sababu huduma ya zahanati iko mbali, tunatoka hapa mpaka Katani Chawi, inafikia hatua tunajifungulia njiani na wakati mwingine mgonjwa akizidiwa tunapata shida kutokana na umbali uliopo wa kupata huduma hii”.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Abdalla Shaib Kaim, ameridhia na kuweka jiwe la msingi mradi huo wa ujenzi wa zahanati katika kijiji hicho, kwani umekidhi vigezo vya ubora unaostahili.
Comments are closed.