Wapuuza mazungumzo ya kusitisha vita Sudan

Ndege za kijeshi za Sudan zinaendelea na mashambulizi ya anga katika mji mkuu Khartoum na miji ya karibu ya Bahri na Omdurman, licha ya mazungumzo ya kusitisha mapigano yanayoendelea Saudi Arabia.

Mapigano ya ardhini pia yanafanyika kati ya jeshi na Kikosi cha dharura (RSF) katika maeneo mawili katikati miji ya Bahri – Shambat na Halfiya.

Mapigano huko Shambat yako karibu na kambi kubwa ya jeshi, wakati vita vya Halfiya vinaonekana kuwa vya kudhibiti daraja muhimu, ambalo kwa sasa liko mikononi mwa RSF.

Advertisement

Mapigano hayo yamewaacha watu wakiwa na hofu kubwa, na kuwalazimu kujificha majumbani mwao.

Lakini watu wengi bado wana matumaini kwamba mazungumzo yanayoendelea nchini Saudi Arabia -ambayo ni ya kwanza baina ya pande hizo zinazohasimiana – yatawezesha kusitishwa kwa mapigano, ingawa mwanadiploamasia ambaye hakutajwa jina ameliambia Shirika la habari la AFP kwamba ‘’hakuna mafanikio makubwa’’ yaliyofikiwa hadi sasa.

Wakati huohuo, jeshi linawashikilia wanaharakati wawili wanaounga mkono demokrasia mjini Bahri, wakiwashtumu kuunga mkono RSF. Wenzao wametaka waachiliwe mara moja, wakisema madai dhidi yao ni ya uongo.

Kamati za upinzani za ujirani – zilizoundwa kufanya kampeni ya demokrasia nchini Sudan – zimekuwa na jukumu muhimu katika kutoa misaada ya kibinadamu kwa wakaazi tangu vita vilipozuka tarehe 15 Aprili.

Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan na kamanda wa RSF Mohamed Hamdan Daglo walikuwa wamefanya mapinduzi kwa pamoja mwaka 2021, lakini sasa wanashiriki katika kupigania mamlaka, na hivyo kuondoa matumaini ya mpito kwa utawala wa kiraia.