WARAIBU wa dawa za kulevya kutoka mikoa mbalimbali, wanaotibiwa katika Hospitali ya Mkoa ya Rufaa, Sekou Toure, wameiomba serikali kuanzisha vituo vya kuwatibu kila mkoa, ili kuwapunguzia makali ya maisha.
Pia wameeleza utayari wao wa kuachana na dawa hizo, wakaomba kupatiwa ajira ili wajikite katika shughuli za kiuchumi, kwa manufaa yao na taifa.
Wamesema matibabu yao, ambayo ni dawa aina ya ‘methadone’ inapatikana mkoani Mwanza tu kwa kanda ya ziwa na mikoa jirani, hivyo kuwalazimu baadhi ya wasio na hifadhi Mwanza kukatisha matibabu.
“Uwepo wa huduma hii kila mkoa si tu kutupunguzia gharama za maisha, bali kuwafikia wengi wanaotamani kuipata, lakini wanashindwa kutokana na umbali. Na dawa hii ni lazima tuimeze kila siku tena mbele ya mtoa huduma,” amesema mmoja wa waraibu, Feisal Seif, kutoka Mkoa wa Shinyanga.
Mwingine kutoka Mkoa wa Tabora, Paschael Bideberi, amesistiza ombi la wao kupatiwa ajira, ili kuepuka kukaa vijiweni, sehemu ambazo ni chanzo kimojawapo cha matumizi ya dawa hizo.
Kama si ajira zinazoendana na fani zao, anapendekeza serikali iwaunganishe na fursa za kilimo zinazotangazwa maeneno mbalimbali ya nchi, kwani tayari ‘methadone’ imewarejesha katika hali ya kawaida, nguvu za kufanya kazi wanazo.
Mkuu wa Idara ya Afya ya Akili hospitalini hapo, Dk Meshack Samuel, amesema muitikio wa vijana kupata matibabu upo na sasa Sekou Toure inahudumia waraibu zaidi ya 300, ambao takribani wote walikua watumiaji wa dawa aina ya ‘heroin’.