WARAJISI wasaidizi wa vyama vikuu vya ushirika kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa kuhusisha pia mikoa ya Singida na Tabora wamesisitizwa na Serikali kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani nakuutumia kwa uzalendo.
Hayo yalisemwa jana na katibu tawala mkoa wa Shinyanga Profesa Siza Tumbo alipokuwa akifugua kikao hicho juu ya majadiliano ya kurudi kwa mfumo wa stakabadhi ghalani na kuanza kutumika.
Profesa Tumbo alisema viongozi wote wa Muungano wa Vyama vya Msingi vya Ushirika watangulize uzalendo, weledi na umakini zaidi katika kutekeleza mfumo huu wa stakabadhi ghalani ili ulete manufaa.
“Lengo la Serikali ni kutaka kuhabarisha juu ya kuanza kwa matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani na kwenda kuwa wazalendo katika utekelezaji wa mfumo huu ili ulete manufaa kama serikali inavyokusudia”alisema Profesa Tumbo.
Profesa Tumbo alisema serikali imeamua kurejesha mfumo huu ili sasa unufaishe vema pande zote kwa mkulima na mlanguzi.
Mrajisi msaidizi mkoa wa Shinyanga Hilda Boniphace aliwakumbusha washiriki kwenda kuanza maandalizi hivi sasa ya namna bora ya utumiaji wa mfumo huu huku akiwasisitiza kwenda kushirikisha makundi yote muhimu katika kuwapatia elimu na taarifa ili wakati utakapofika iwe rahisi katika utekelezaji wake.
Meneja uendeshaji soko la bidhaa Tanzania TMX Augustino Mbulumi alisema stakabadhi ghalani lengo lake kumsaidia mkulima na kuwa na soko la uhakika na kuuza kwa bei ya soko na kiwa katika ushindani wa kidigital.
Ofisa udhibiti ubora kutoka bodi ya usimamizi wa stakabadhi za ghala Tanzania Witness Temba alisema wamekuwa wakithibiti mazao katika utunzaji ili yawe na ubora.
Robert Nsunza kutoka Masoko na uwekezaji tume ya maendeleo ya ushirika Tanzania alisema ushirika lazima umlinde mkulima na kumpatia elimu ya namna ya kuingia kwenye ushindani wa soko na stakabadhi ghalani iwepo kwa manufaa ya wote isimnyonye mtu.