WAZIRI Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba amesema viongozi wa vyama vya siasa nchini wana jukumu la kuhakikisha misingi ya amani na uhuru iliyowekwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumanne wakati wa kongamano la tathmini ya shughuli zinazofanywa na Wakfu wa Mwalimu Nyerere (MNF) tangu kuanzishwa kwake miaka 25 iliyopita, Jaji Warioba amesema umoja wa kitaifa utaimarika zaidi ikiwa wanasiasa watazingatia hilo.
Jaji Warioba amedai kwamba vyama vya siasa vimekuwa chanzo cha kuwagawa wananchi jambo ambalo sio zuri kwa siasa yetu.
“Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 wa mfumo wa vyama vingi kule Zanzibar watu waligawanyika na ilifika hatua ya kususiana, Ilichukua muda kuwaunganisha tena kama ilivyokuwa awali. Hatua hii itasaidia kuwaunganisha wananchi badala ya vyama vya siasa kuwagawa wananchi kwa itikadi ya vyama vyao.
“Ifike wakati tufanye jitihada kama walizozifanya visiwani Zanzibar kwa viongozi wote wa kisiasa kukubali kulinda misingi iliyowekwa ya uhuru wa nchi na wananchi.
Jaji Warioba ambaye alikuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya ameongeza kuwa, viongozi wa vyama vya siasa waache tabia ya kuwagawa wananchi.
“Viongozi wetu walikuwa mstari wa mbele kuweka misingi ya umoja na amani hivyo tuendelee kuwaunganisha wananchi na kuwa na siasa nzuri yenye umoja na amani kufuata yaliofanywa na waasisi.”