MASHIRIKA, watu binafsi na taasisi mbali mbali leo zimesaini makubaliano ya kumaliza ndoa za utotoni nchini, ambapo imeelezwa msichana mmoja kati ya watatu anaolewa kabla ya kufikisha miaka 18
Tayari Saini 10, 663 kutoka mashirika, taasisi na watu binafsi zimekusanywa katika kampeni iliyozinduliwa leo Septemba 17, 2022 jijini Dar es Salaam ya kutokomeza ndoa za utotoni inayoendeshwa na Shirika Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF).
Kampeni hiyo iliyopewa jina la ‘Binti’ inalenga kupata uungaji mkono wa jamii, ili kuongeza umri wa msichana kuolewa na kubadilisha mtazamo wa jamii, kuhusu umuhimu wa mtoto wa kike.
Zlatan Millisic, Mratibu Mkazi wa UN upande wa Tanzania, akizungumza katika uzinduzi huo amesema UN Tanzania inasaidiana na serikali kuhakikisha inatokomeza ndoa za utotoni.
Amesema athari anazokumbana nazo msichana anapokuwa na hali ya kutarajia kukatisha masomo, utoto, na ndoto zao ili kuolewa, inadhuru afya yao ya akili, na wanakabiliwa na mduara wa ukatili, unyanyasaji, changamoto za kiafya na umaskini.
“Kati ya wasichana watatu, mmoja anaolewa chini ya umri wa miaka 18, hii inamfanya msichana apoteze fursa za elimu na ujuzi wa kazi, kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi, (vvu), fistula au magonjwa ya zinaa, kunyanyasika kisaikolojia, kimwili, kijinsia na hivyo kudhuriwa kwa haki na utu wao.
“Hili lazima tulikemee kwa kuwa linaathiri kuyumba kiuchumi na kudumu katika umasikini, vifo vya watoto wachanga na watoto wa kike pindi wanapojifungua kwa kuwa viungo vyao vya uzazi bado havijakomaa pia inaongeza vifo vya wajawazito na kuharibika kwa mimba,” amesema Zlatan.
Amesema kuzuia ndoa za utotoni ni mwanzo wa kukabiliana na masuala mengine makubwa yanayowahusu watoto na matarajio ya vijana na fursa za maisha, thamani ya wasichana katika jamii, kuvunja mzunguko wa umasikini, na kuhakikisha nafasi za vijana kama wakala wa mabadiliko.
“Tunahitaji kuangalia kwa karibu fursa ambazo wasichana nchini Tanzania wanazikosa kutokana na ndoa za utotoni,” amesema.
Kwa mujibu wa takwimu za UNICEF, inakadiriwa kuwa, wasichana watatu kati ya 10 nchini wanaolewa wakiwa bado watoto, na kuifanya Tanzania kushika nafasi ya 11 kwa ndoa za utotoni duniani.
Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inaweka miaka 18 kuwa umri mdogo ambao wavulana wanaruhusiwa kuoa, lakini imeweka umri wa miaka 15 kwa wasichana kuolewa kwa ridhaa ya wazazi, sheria hiyo wadau wametaka serikali ifanyie marekebisho, kwani inapingana na wakati na haipo wazi, ikishindwa kufafanua mtoto ni nani.
Kwa upande wa Mhariri wa Habari wa gazeti la Mwananchi na mwakilishi wa Jukwaa la Wahariri (TEFF), Lilian Timbuka amesema vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kutoa elimu, ili kusaidia kutokomeza ndoa za utotoni.
Amesema kwa kuwa wanaoathirika zaidi ni wasichana wanaoishi pembezoni, hivyo juhudi kubwa za wamiliki na waandishi wa habari ni kupaza sauti kuwasemea wale ambao hawawezi kujisemea.
“Sauti isiyo na sauti inapazwa na vyombo vya habari, lakini tunahamasisha kampeni hizi ziende zaidi vijijini, huko ndiko athari hizi zinatokea zaidi na wazazi, walezi na wasichana wenyewe hawana taarifa,” amesema Timbuka.
Mwakilishi wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini, na Mkuu wa jimbo la Magharibi-Dayosisi ya Mashariki na Pwani KKKT, Anta Muro, amesema viongozi wa vyombo vya dini wanaunga mkono kampeni hiyo, kwa lengo la kupambana na tatizo la watoto kuolewa katika umri mdogo.