Wasaini ushirikiano utafiti wa masoko

KAMPUNI ya Huduma za Meli (MSCL) na Wakala wa Uwezeshaji wa Usafiri wa Ushoroba wa Kati (CCTTFA), zimesaini makubaliano ya ushirikiano (MoU), kwa ajili ya kuwezesha tafiti  za masoko mapya katika Ziwa Victoria na Tanganyika.

Kwa makubaliano hayo, CCTTFA inatoa zaidi ya Sh millioni 165, kiasi ambacho kitatumika pia kwa shughuli za mapitio ya tozo za MSCL, ili kupata viwango vinavyoendana na hali ya soko ya sasa.

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa MSCL, Eric Hamissi, kwa kuanzia tafiti zitafanyika kwa masoko ya Jinja (Uganda) na Kisumu (Kenya) katika Ziwa Victoria na Zambia kwa Ziwa Tanganyika.

“Tutaendelea kuangalia masoko mengi zaidi ikiwemo ya DRC Congo, Bujumbura na mengine mengi. Tafiti ndizo zitakazotuelekeza twende wapi,” amesema wakati wa kusaini makubaliano.

Amefafanua kwamba ufadhili huo ni muendelezo wa makubaliano yaliyosainiwa Septemba, 2020, ambapo wakala ulitoa zaidi ya Sh million 209, kwa ajili ya mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa MSCL, ili watekeleze majukumu yao ipasavyo.

“Kwa hiyo jumla ya kiasi cha mkataba wa leo na wa awali imekua Sh 375, 070, 000,” amesema.

Katibu Mtendaji wa CCTTFA, Okandju Flory, amesema ushirikiano baina ya pande hizo mbili utaendelezwa, ili kuboresha usafirishaji katika maziwa hayo makuu.

 

Habari Zifananazo

Back to top button