Wasaini ushirikiano wa malikale
TAASISI ya Makumbusho ya Taifa ya Tanzania na Makumbusho na Mambo ya Kale Zanzibar, zimesaini mkataba wa ushirikiano katika uhifadhi wa malikale nchini.
Mkataba wa ushirikiano baina ya makumbusho hizo umesainiwa leo Dar se sSalaam na wakuu wa taasisi hizo mbili.
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa ya Tanzania, Dk Noel Lwoga alisaini mkataba huo kwa niaba ya taasisi yake na kwa upande wa Zanzibar, mkataba huo ulisainiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale, Maryam Mansab.
Katika mkataba huo taasisi hizo zimekubaliana kushirikiana katika maeneo ya uhifadhi, utafiti, utalii wa malikale, utoaji elimu kwa jamii, mafunzo na kujenga uwezo kwa watumishi na kufanya matukio na maonesho ya pamoja.
Pia viongozi wa wizara walishuhudia utiaji saini huo akiwepo Dk Amina Amer, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar na Bernard Patrick, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Wizara ya Maliasili na Utalii aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Hassan Abbas.