DAR ES SALAAM: Wasanii na wadau sanaa wametakiwa kufanya kazi kwa makubaliano kwa kuandikishana mikataba, itakayoleta amani, upendo ushirikiano na umoja ili kuepuka migogoro baina yao.
Hayo yamezungumzwa na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ alipokutana na msanii wa Bongo fleva, Kayumba Juma baada ya kuona malalamiko yake akidai kudhulumiwa fedha kiasi cha Sh million nne na mwongoza video za Bongo fleva Erick Mzava.
Mwana FA amekutana na msanii huyo na kutatua mgogoro huo kwenye ofisi ndogo za wizara zilizopo Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam ambapo ameisikiliza changamoto hiyo na ameahidi kufanyia kazi ndani ya muda mfupi.
Kayumba aliandika kupitia ukurasa wake Instagram akidai kuwa amedhulumiwa fedha kiasi cha Sh milioni nne na laki moja ambazo alizitoa kwa ajili ya kufanyiwa video ambayo haikufanyika kama walivyokuwa wamekubaliana.