Wasanii watakiwa kuchangamkia fursa za mikopo
WASANII, wadau mbalimbali wa sanaa mkoani Mtwara wametakiwa kuchangamkia fursa ya mkopo wa takribani Sh bilioni 20 iliyotolewa na serikali kupitia sekta ya utamaduni na sanaa ili kujiinua katika kazi zao.
Akizungumza wiki hii katika mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uwezo zaidi wasanii na wadau wa sekta hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa, Nyakaho Mahemba amesema mfuko huo umeanzishwa na serikali kwa ajili ya kuwainua kiuchumi wasanii ikiwa ni pamoja na kusaidia ununuzi wa vifaa vya kuzalishia kazi za wasanii hao na fedha za uendeleshaji wa uzalishaji.
Amesema serikali inatambaua kwamba changomoto ya wasanii hao ni mitaji hivyo wanashindwa kuzalisha kazi bora kutokana na ukosefu wa mitaji ambapo baadhi ya changamoto inayowakumba wasanii ikiwemo kuanzisha, kukuza, elimu na kuendeleza kazi hizo, serikali hiyo baada ya kubaini hilo inatoa mkopo wa masharti nafuu kwa mtu mmoja mmoja, vikundi na makampuni ili waweze kuzalisha kazi bora zitazokidhi soko la ndai na nje.
‘’Ili kutatua hiho serikali imeanzisha mikopo ya masharti nafuu na kiwango cha chini cha mkopo huo ni Sh 100,000 na cha juu Sh milioni 100 na riba yetu ni nafuu sana ambayo asilimia 9 inayotozwa katika salio la mkopo, tunamshukuru Rais wetu wa awamu ya sita Dk Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuiheshimisha sekta hii dhamila yake ni kuzalisha ajira nyingi katika nchi yetu kupitia sekta hii kwa kutambua kwamba vijana wengi wanaangukia katika sekta hii’’.amesema
Amesema serikali imetenga fedha Sh bilioni 20 mwaka huu wa fefha 2023/24 kwa ajili ya kutoa mikopo mipya katika sekta hiyo na katika fedha hizo mpaka sasa tayari wameshatoa Sh bilioni 1 kwa baadhi ya mikoa ikiwemo Dar es salaam, Iringa, Dodoma, Njombe, Morogoro na wanategeme kutoa tena kwenye mikoa mingine Agosti mwaka huu hivyo wamekuja mkoani humo ili kutoa elimu kwa jamii kuhusu kuchangamkia fursa hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Hanafi Msabaha amewasisitiza wasanii mkoani humo kuonyesha uwaminifu wakati wanapotumia mikopo hiyo kama ilivyokusudiwa na serikali huku akiupongeza mfuko huo kwa jitihada hizo kwani wanaenda kutengeneza matajiri wengi zaidi kupitia sekta hiyo.
‘’Ni fursa kubwa ambayo hatujawahi kuipata ni wewe kujipanga andiko lako zuri ukatekeleze majukumu haya kama ilivyotarajiwa, ukikopa fedha urejeshe ili wasanii wengine waweze kukopa usipofanya hivyo utaufanya mfuko ushindwe kuendelea na wasanii wengine hawatapata fedha ukikopa usibadili mawazo ili kuifanya ajira ya kudumu tofauti na iliyokuwa inatafsiliwa mwanzo’’,amesema Msabaha
Msanii mkoani humo, Mwanaisha Bakari ameipongeza na kuishukuru serikali kwa kuwajali wasanii hao na kuwaletea mfuko huo ambao utawavusha katika kazi yao hiyo kutoka sehemu moja kwenda nyingine ikiwa kazi hizo sasa zinaenda kuwa miongozi mwa fursa zilizopo katika mkoa huo.