Wasanii zaidi ya 6000 kufungiwa

BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limewapongeza wasanii Nassibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Ali Salehe ‘Alikiba’ kwa kuongoza kwa kufuata sheria zao za ukataji vibali huku wakitangaza kuwafungia zaidi ya 6000 walioshindwa kufuata sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Katibu Mtendaji wa Basata Dk Kedmon Mapana alisema Diamond na Alikiba ni wasanii waliofanya vizuri mwaka 2023 hivyo, atawatunuku vyeti kwa kutambua mchango wao katika kuzingatia sheria za Basata.

Aidha, wengine wanaoongoza ni kundi la sarakasi la Ramadhan Brothers, DJ Hamad Hassan, baa zilizofanya vizuri ni Klabu Element na Twelve 45 na makampuni ni Food and Beverage master Limited na Synergy Concept Limited.

“Hawa walikuwa wakialikwa nje lazima waje wakate vibali, wakileta wasanii wanawakatia vibali lazima tuwapongeze na kuwapa vyeti ili kutoa motisha kwa wengine kujitahidi,”alisema.

Katika wasanii zaidi ya 6000 ambao wanaweza kufungiwa au kufutiwa usajili kati ya hao, 4989 ni vikundi vya sarakasi, dansi na muziki, 1548 ni mapromota ambao wamejisajili lakini hawaonekani na 227 ni taasisi zinazofanya biashara za sanaa.

Dk Mapana alisema ifikapo Desemba 30, hao wanaokusudiwa kufungiwa wanatakiwa wafike Basata kuhuisha vibali vyao na wale wasiofuata sheria watafutiwa au kutozwa faini kuanzia Sh milioni moja hadi tatu.

Alisema ikiwa kuna waliokwama pia, wajitokeze wazungumze ili kuweka mambo sawa kwa manufaa ya sanaa.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button