Washauri jamii kugeukia kilimo ikolojia

Kilimo cha Ikolojia

WADAU wa kilimo ikolojia wameshauri jamii kuanza jitihada ya kukuza sekta hiyo ili kujenga mazingira endelevu yanayoweza kustahimili mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kuikumba dunia kwa sasa na kusababisha changamoto nyingi.

Walisema kutokana na mabadiliko ya tabianchi jamii inatakiwa kuchukua hatua katika kuwezesha kilimo ndelevu kwa kuepuka athari zinazochangia uharibifu wa mazingira.

Mtaalamu wa Mnyororo wa Thamani wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali lenye kujishughulisha na Kilimo (ANSAF), Owen Nelson alisema jana jijini Mwanza kuwa kunahitajika kuwepo kwa sera ambayo itachangia kukuza kilimo hicho kwa sasa.

Advertisement

Alisema kilimo ikolojia ni rafiki kwa mazingira na viumbe hai hivyo umefika muda kwa taifa kuendeleza jitihada za kukiinua kwani kuna madhara ambayo yamekuwa yakiendelea kukabili mazingira na uhai wa viumbe kutokana na kuwepo kwa matumizi ya viuatilifu ambavyo vina madhara.

Nelson alisema kunahitajika ushirikiano baina ya wadau wa maendeleo katika sekta ya kilimo ili kujifunza kuwa na mtazamo wenye tija kwa ajili ya kuwezesha sekta hiyo kutumika ili kuleta uendelevu wa mazingira na viumbe wake.

“Kuwepo kwa uelewa wa pamoja juu ya umuhimu wa kilimo ikolojia (kisichotumia kemikali) kutasaidia kuibua mijadala muhimu na hatimaye kuwepo jicho la kisera kwenye sekta hiyo,” alisema Nelson.

Alisema kupitia ANSAF wamekuwa na majukwaa makubwa ya kilimo ikolojia katika mikoa ya Kusini, Kati na Kaskazini kujadili umuhimu wake kwa sasa kwani dunia inaendelea kukabiliana na changamoto ya ukame, mafuriko na madhara ya baadhi ya viuatilifu katika ardhi.

Kikao hicho cha kilimo ikolojia kilikuwa na kaulimbiu isemayo “Maendeleo ya Kilimo kwa maslahi ya wazalishaji wadogo”.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Idara ya Ugani na Maendeleo ya Jamii, Dk Siwel Nyamba alisema kuwepo kwa kilimo hicho ni muhimu kwani kitapunguza matumizi yasiyo ya lazima ya kunyunyizia viuatilifu vyenye sumu.