Washauri kusoma nje kuendana na fursa za ajira

TAASISI inayounganisha wanafunzi kwenda kusoma nje ya nchi ya EduKwanza imewataka wanafunzi wasiogope kwenda kusoma nje kwa sababu kuna fursa mbalimbali kulingana na soko la ajira.

Pia imesema kuwa wanahakikisha hakuna usiri katika huduma wanazotoa na wanafunzi wanawapeleka katika vyuo ambavyo ni salama kwenye ulinzi, afya na mazingira bora ya kusomea.

Ofisa Mdahili wa masomo kutoka EduKwanza, Jimmy Samwel amesema hayo Julai 23,2023 baada ya kuhitimishwa kwa maonesho ya vyuo vikuu yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

Advertisement

Amesema katika maonesho hayo, wamesajili zaidi ya wanafunzi 100 ambao wana nia ya kwenda kusoma nje ya nchi huku wengine 200 wakitaka taarifa namna ya kupata fursa hiyo ya masomo.

Samwel amesema kuwa moja ya vigezo vinavyotakiwa na waajiri ni uzoefu hivyo, vyuo wanavyoshirikiana navyo vinatoa mafunzo ya nadharia na vitendo kwa kuwaunganisha wanafunzi na Kampuni mbalimbali ili kuwa na mchango katika maendeleo ya nchi.

Ametoa mfano wa vyuo vilivyopo Canada kwamba nchi hiyo imekuwa ikishirikiana na Kampuni na mashirika mbalimbali ili wanafunzi wapate fursa ya mafunzo kwa vitendo na wanapomaliza wanakuwa na uzoefu unaotakiwa kulingana na mahitaji ya soko la ajira.

Pia amesema vyuo vya nje hutoa udhamini wa masomo kuanzia asilimia 10 hadi 50 na vingine hutoa asilimia 100 ikiwemo India ambapo wanafunzi husoma bure isipokuwa huchangia gharama ya malazi na chakula.

“Tunawasaidia wanafunzi kupata vyuo nje ya nchi na kuwapa maelekezo kuhusu masomo mbalimbali ambayo wanaweza kuyasomea. EduKwanza imeanza mwaka 2021 na tunashirikiana na vyuo zaidi ya 500 ulimwenguni,” amesema Samwel.

Amesema vyuo hivyo vinatoa kozi mbalimbali ikiwemo udaktari, uhandisi, uhasibu, uanasheria na mengine.

“Vyuo ambavyo tunashirikiana navyo ni kutoka bara la Ulaya, Amerika, Asia nchi za Kiarabu na Uingereza. Hatuna utaratibu wa kuwatoza wanafunzi fedha kwa lengo la kupata huduma ya ushauri wa vyuo na kozi badala yake tunatoza Dola 200 endapo mwanafunzi atataka kujiunga na moja ya vyuo wanavyoshirikiana navyo,” amesisitiza.

Ameongeza kuwa “Tunashukuru kupitia maonesho haya tumepata mwitikio mzuri wa Watanzania kwa wale wanaohitaji kwenda kusoma nje ya nchi na kati ya vyuo tulivyovialika wamepata wanafunzi kwa ajili ya kuanza masomo mwaka huu.”

Samwel amesema wanatarajia mwaka ujao wataalika vyuo vingi zaidi kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujiunga na vyuo vyao kupitia maonesho hayo.

3 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *