WAKULIMA, wadau mbalimbali Kanda ya Kusini, katika mikoa ya Lindi, Ruvuma na Mtwara wametakiwa kuzalisha na kutumia chakula kitokanacho na mazao ya asili ili kuboresha afya ikiwemo kuongeza lishe na kutokomeza udumavu katika jamii.
Akizungumza wiki hii katika maonesho ya Nane nane mwaka 2023 yanayoendelea katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi kwenye maonesho ya mbegu za asili na matumizi ya vyakula vya asili, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas amesema wananchi wapende kula vyakula hiyo kwa ajili ya afya zao.
Maonesho hayo yamefanyika katika banda la taasisi ya SWISSAID nchini iliyojikita kufundisha Wakulima Kanda ya kusini namna bora ya kuzalisha mbegu hizo na mazao ya asili ambayo yanafaida kubwa kwa jamii.
Aidha,amewakumbusha wananchi hao kuhusu suala zima la matumizi mbegu hizo kwa ajili ya usalama wa afya, lishe, pamoja na vyakula.
Amesema kumekuwepo kwa janga la ukosefu wa nguvu za kiume kwa baadhi ya wanaume hivyo warudi kwenye matumizi ya kula vyakula hivyo kama tiba mbadala.
“Sasa turudi kwenye matumizi ya kula vyakula vya asili kama tiba mbadala ya nguvu hizo za kiume badala ya kujikita kutafuta madawa yenye kemikali ambayo baada ya kutibu kudhohofisha afya zetu”,amesema Abbas
Amesema serikali kupitia Wizara ya kilimo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo imeandaa mikakati ya kilimo kwa kutoa mwanga juu ya uendeshaji wa kilimo hai na uhakika wa uzalishaji wa chakula salama na chenye utoshelevu wa lishe bora nchini.
Mkurugenzi wa Swissaid, Betty Malaki amesema taasisi hiyo inafundisha wakulima kuanzia uzalishaji, utunzaji wa mazao na kuweka akiba ya mbegu ili kurahisisha upatikanaji wa mbegu kwa jamii.
Mkulima kutoka mkoani Lindi, Hawa Mohamed amepongeza jitihada hizo zinazofanywa na serikali imewaongezea tija kubwa ya wao kuweza kuzalisha mbegu hizo ambazo sasa wanapata chakula cha asili kwa ajili ya afya zao.