VYAMA vya wafanyakazi na taasisi za umma na binafsi zimeshauriwa kuweka nguvu eneo la mafunzo kuhusu sheria za kazi kwa wafanyakazi ili kupunguza migogoro sehemu ya kazi.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Ufundi Stadi, Ushauri, Habari na Utafiti (RAAWU), Joseph Sayo alisema hayo jijini Mwanza alipofungua mafunzo ya viongozi wa vyama vya wafanyakazi na menejimenti wa chama hicho.
Sayo alisema njia muhimu ya kuwezesha utendaji wenye ufanisi sehemu ya kazi, kunahitajika uelewa wa pamoja kuhusu umuhimu wa chama cha wafanyakazi na sheria za kazi ikiwemo ya Utumishi wa Umma Namba 8 ya Mwaka 2002 na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6 ya mwaka 2004.
Alisema sheria zote hizo ni za muhimu wafanyakazi kuzijua hasa viongozi wa wafanyakazi na menejimenti ili kwa pamoja kuzuia migogoro sehemu ya kazi.
Sayo alizishukuru taasisi zilizowezesha viongozi wengi wa wafanyakazi kuhudhuria semina hiyo na kuomba taasisi zenye kusuasua, zitekeleze takwa hilo la kisheria linalodondokea kwenye eneo la mafunzo katika bajeti za taasisi.
Kuhusu mada za mafunzo katika semina hiyo, alisema mbali na sheria za kazi, washiriki watajifunza kuhusu mabadiliko ya tabianchi, kikokotoo, ujasiriamali na wajibu wa vyama vya wafanyakazi.
Katibu Mkuu huyo wa RAAWU Taifa aliishukuru serikali kwa kuwapandisha vyeo wafanyakazi walioacha kupandishwa muda mrefu na ahadi yake ya kuendelea kufanyia kazi changamoto zinazowakabili wafanyakazi ili kuwapunguzia gharama za maisha.
Sayo ambaye alichaguliwa mwaka jana kushika nafasi hiyo, alisema RAAWU inaendelea kushirikiana na serikali na vyama vingine vya wafanyakazi kuhakikisha maslahi ya wafanyakazi yanazingatiwa.
Alitumia nafasi hiyo kuiomba serikali kufanyia kazi ripoti ya vyama kuhusu mapendekezo ya Bodi za Mishahara kwa Sekta Binafsi ili na wafanyakazi wa sekta hiyo waweze kupandishiwa mishahara kwani tangu mwaka 2013 ndio tamko la mwisho lilitolewa na serikali la kupanda mishahara rasmi kwa sekta hiyo.
Ofisa Rasilimali watu wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Catherine Chamungwana na Katibu wa RAAWU TSN, Mbonile Burton kwa nyakati tofauti walisema wanatarajia kujifunza mengi katika mafunzo hayo hasa sheria za kazi na kanuni zake.