Washauri serikali itumie wataalamu kukuza uchumi

Washauri serikali itumie wataalamu kukuza uchumi

SERIKALI imeshauriwa kutumia wataalamu na watafiti kutoka katika vyuo vikuu kufanya utafi ti kujua matatizo halisi yanayowakabili wananchi kama sehemu ya kuweka mipango ya kukuza uchumi.

Hivi karibuni Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alitangaza malengo sita ya uchumi kwa mwaka wa fedha 2023/24 ukiwamo ukuaji wa pato halisi la Taifa kufikia asilimia 5.2 mwaka 2023 kutoka matarajio ya ukuaji wa asilimia 4.

7 mwaka 2022; Dk Mwigulu alitaja malengo mengine ni kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia kati ya asilimia 3.0 hadi asilimia 7.0 katika muda wa kati na mapato ya ndani (ikijumuisha mapato ya halmashauri) kufikia asilimia 14.9 ya Pato la Taifa mwaka 2023/24.

Advertisement

Wabunge walielezwa malengo mengine ni mapato ya kodi kufikia asilimia 12.1 ya Pato la Taifa mwaka 2023/24 kutoka matarajio ya asilimia 11.5 mwaka 2022/23, nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) kuwa chini ya asilimia 3.0 ya Pato la Taifa mwaka 2023/24 na kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.

Mhadhiri na Mtaalamu wa Uchumi kutoka katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine, Dk Isack Safari aliishauri serikali ifanye utafiti ili kujua hali halisi ya maisha ya wananchi kwa kutumia wataalamu wa utafitio kutoka vyuo vikuu.

Dk Safari alisema njia rahisi ya kuyafikia malengo hayo ni kupanga mipango ya muda mfupi ikiwa ni pamoja na kurejesha na kusimamia nidhamu ya watendaji hali itakayookoa fedha nyingi ambazo zingetumiks katika maeneo mengine.

“Suala lingine ni kuharakisha miradi ya kimkakati ikamilike na kuanza uzalishaji hali itakayoongeza fedha ambazo mwisho wake ni kukuza mapato ya nchi pamoja na wananchi kwa ujumla,” alisema.

Dk Safari alisema ili kupunguza mfumuko wa bei, serikali inapaswa kuongeza uzalishaji wenye tija kwa kuzalisha mazao ya kutosha na yenye ubora utakaosaidia kupunguza mfumuko wa bei hapa nchini.

Alisema kuna wakati uchumi wa nchi inatetereka kutokana na matatizo ya nje ya nchi hivyo ili hali hiyo isitokee serikali ipunguze utegemezi kutoka nje katika bidhaa yakiwamo mafuta ya kula kwa kuweka mkazo katika uzalishyaji wa ndani hususani kwa kutumia mazao ya alizeti, ufuta, karanga na mawese.

Mchambuzi wa Masuala ya Uchumi ambaye pia ni Mhadhiri wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Vicent Leyaro alisema kabla ya kutekeleza mipango ya kukuza uchumi, serikali inapaswa kuwa na majibu ya namna ya kukabili majanga yanayotingisha uchumi kama ukame, vita vya Ukraine na janga la Covid- 19.

Alishauri kuwa ili kupata majibu sahihi ni lazima itumie wataalamu wake kufanya utafiti wa matatizo yanayowakabili wananchi hali itakasaidia kupatikana na suluhu ya kudumu ya tatizo yanayoisumbua jamii na uchumi kwa ujumla.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi na siasa, Profesa Humphrey Moshi alisema mipango ya serikali kukuza uchumi mwaka 2023/24 ni mizuri lakini inaweza kuleta shida katika usimamizi.

Profesa Moshi alisema njia rahisi ya kutekeleza mipangp hiyo ni kuboresha kilimo cha umwagiliaji ili kuwezesha uzalishaji wa mazao ili kuepuka kuagiza mazao kutoka nje ya nchi.

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *