Washauri ujenzi vyumba vya kunyonyeshea

VIONGOZI wa dini wameshauri ujenzi wa vyumba maalumu katika maeneo mbalimbali yanayokutanisha watu vitakavyotumiwa bure na akinamama kunyonyesha watoto wao kama moja ya mikakati inayolenga kulinda, kuimarisha na kuendeleza unyweshaji maziwa ya mama kwa mtoto.

Maeneo hayo ni pamoja na ya kazi, biashara, stendi, nyumba za ibada kama makanisa na misikiti na mengine yote yanayokusanya watu kwa shughuli mbalimbali za kijamii na maendeleo wakiwemo akinamama wanaonyonyesha.

Wametoa ushauri huo mjini Iringa katika warsha ya siku moja ya viongozi hao na wa kimila iliyohusisha Wizara ya Afya, Wizara ya Kilimo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) katika kuadhimisha Wiki ya Unyonyeshaji Duniani.

Mmoja wa viongozi hao, Mchungaji Modest Pesha kutoka Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) alisema; “Baadhi ya watoto wachanga wamekuwa wakipoteza haki yao ya msingi ya kupata maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita kwasababu ya mama zao kuwa katika mazingira yanayoweza kuwafanya waone aibu au washindwe kuwanyonyesha.”

Alisema wakati umefika kwa sera na sheria ya mtoto nchini kufanyiwa maboresho yatakayofanya iwe ni haki ya msingi kwa mtoto kupata maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita.

“Kujengwa kwa chemba maalumu za kunyonyeshea watoto katika maeneo hayo kutasaidia kuwasitiri mama zetu na kutawawezesha watoto wao kupata haki yao ya kunyonya bila wasiwasi katika mazingira ambayo mama anakuwa nje ya nyumbani kwake akiendelea na shughuli zingine zikiwemo za kujipatia kipato,” alisema.

Mratibu wa Afya wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Dk Saleh Abdalah alisema suala la lishe na unyonyeshaji limetajwa katika kitabu kitakatifu cha dini hiyo na akaiomba serikali kulifanyia kazi pendekezo hilo huku akiwaomba waajiri katika sekta ya umma na binafsi watengeneze sera zitakazomuwezesha mama amnyonyeshe mtoto wake kwa kipindi chote kinachotakiwa.

Sheikh wa Iringa Mjini, Salum Suleiman alitilia mkazo suala la unyonyeshaji akisema baada ya miezi sita ya mtoto kunyonya maziwa pekee ya mama, anatakiwa kuendelea kunyonyeshwa hadi miaka miwili.

“Suala la lishe na unyonyeshaji mkoani Iringa linafanywa kwa kiwango cha chini, ombi letu waislamu wazingatie maandiko yanavyotaka katika mambo hayo hatua itakayoiwezesha jamii kuwa yenye afya na bora,” alisema.

Kwa upande wake Mchungaji Upendo Sanga wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa alisema unyonyeshaji umeendelea kuwa changamoto kubwa kwa jamii ya kitanzania kwasababu ya ongezeko la kina mama wanaobanwa na shughuli za kikazi katika sekta za umma na binafsi.

“Tunapendekeza kuwe na chemba za unyonyeshaji katika maeneo ya kazi, pamoja na pendekezo hilo ni muhimu sana kwa waajiri kuwa na sera zitakazowezesha jambo hilo kupata mafanikio,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Akinamama wa Kiislamu (JUWAKITA) Iringa, Semeni Ngenzi aliwakosoa akinamama wa siku hizi akisema staili zao za maisha zinachangia kuwanyima watoto wao haki ya kunyonya kama inavyoshauriwa kitaalamu.

“Akinamama wa siku hizi hawawanyosheshi watoto wao kwa kuzingatia muda unaoshauriwa kwa kile wanachodai hawataki matiti yao yaanguke, hii sio sawa kwa afya ya mtoto,” alisema.

Naye Afisa Lishe wa FAO, Stella Kimambo alizungumzia umuhimu wa chemba hizo huku akiomba sekta binafsi kama ilivyo kwa sekta ya umma kuwa na miongozo ya kisheria itakayotoa haki ya uzazi kwa akina mama ikiwemo suala la likizo ya uzazi.

“Wito wetu pia kwa akinamama wasio na ajira au wakulima vijijini-akina baba watimize majukumu yao kwa kuhakikisha wanawapatia lishe bora lakini pia wanawapunguzia majukumu yao majumbani na shambani,” alisema.

Afisa Kilimo Mkuu na Mratibu wa Lishe wa Wizara ya Kilimo, Margaret Natai alisema sekta ya kilimo ina mchango mkubwa katika kumuwezesha mama kupata lishe bora itakayomsaidia kutoa maziwa ya kutosha na yenye virtubishi vyote kwa mtoto wake.

“Watanzania wakielimishwa ipasavyo, tutapunguza sana tatizo la lishe na udumavu kwasababu kwa nchii tatizo sio vyakula, vyakula vipo, changamoto ni namna vyakula hivyo vinavyotumiwa,” alisema.

Afisa Lishe wa Mkoa wa Iringa, Anna Patrick alisema wakati takwimu za kitaifa zikionesha wastani wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee ni asilimia 64, mkoa wa Iringa umevuka kiwango hicho ukiwa na asilimia 66.

Pamoja na kuendelea kupata mafanikio katika unyonyeshaji Patrick alisema mkoa wa Iringa ndio unaoongoza nchini kwa kuwa na asilimia 56.9 ya udumavu wa watoto.

“Udumavu mkoani Iringa unazidi kuongezeka. Kwa kushirikiana na wadau wetu mbalimbali kwasasa tupo kwenye hatua za kutafuta visababishi, utafiti huo utatupa picha halisi ili tuendelee kuchukua hatua za kukuabiliana nao,” alisema.

Afisa Lishe kutoka Wizara ya Afya, Elieth Rumanyika alizungumzia dhana ya maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji ambayo hufanyika Agosti 1 hadi 7 ya kila mwaka akisema yanatoa kwa jamii fursa ya kupata elimu juu ya umuhimu wa unyweshaji wa maziwa ya mama kwa mtoto.

Alisema maziwa ya mama ni chanzo kamili na chenye uwiano cha lishe kwa watoto, na uwapa virutubishi vyote muhimu, kingamwili, na vimeng’enya kwa ukuaji na ukuaji bora.

“Yana protini muhimu, mafuta, wanga, vitamini, na madini ambayo yanakuza mfumo wa kinga wenye afya, maendeleo ya ubongo, na ustawi wa mtoto kwa jumla,” alisema.

Alisema viongozi wa dini wakipata taarifa sahihi kuhusiana na umuhimu wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama, watafikisha kwa usahihi ujumbe huo na matokeo yake yanaweza kuwa makubwa kwakuzingatia jinsi wanavyoaminika katika jamii.

“Miezi sita ya mwanzo mtoto anatakiwa kunyonya maziwa ya mama pekee. Na baada ya hapo mtoto ataendelea kunyonya hadi miaka miwili huku akipewa chakula cha nyongeza kinachozingatia lishe bora,” alisema.

Mwisho.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Alice Arm
Alice Arm
1 month ago

Looking for Alice Arm seams is the worldwide indigenous nuts for all to nil to everyone.

https://globaljournals.org/GJMBR_Volume15/5-Mining-and-First-Nations.pdf

Back to top button
1
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x