WADAU wa demokrasia nchini wamesisitiza suala la rushwa ya ngono kuingizwa katika sheria ya vyama vya siasa ili kuweka mkazo wa udhibiti wa vitendo hivyo vinavyorudisha nyuma mustakabali wa wanawake katika siasa.
Aidha, wamesema pia sheria ibainishe wazi jinsi vyama vinavyotumia ruzuku inayotolewa kwao kwa ajili ya kusaidia wanawake kwenye siasa.
Mapendekezo hayo yalitolewa Dar es Salaam jana katika mkutano mkuu maalumu wa Baraza la Vyama vya Siasa unaoshirikisha wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa kujadili miswada ya sheria za uchaguzi na wa sheria za vyama vya siasa.
Akizungumza, Mwakilishi kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar, Musa Kombo alisema udhibiti wa rushwa ya ngono kwenye vyama vya siasa ni muhimu kuwepo kwenye sheria ili kukabiliana na suala hilo.
Alisema rushwa ya ngono imekuwa ikiwasumbua wanawake na zaidi kuwatia hofu ya kushiriki kwenye chaguzi mbalimbali.
“Suala la rushwa ya ngono limekuwa likitajwa katika vyama vya siasa, ambapo kwa upande mmoja hutia hofu kwa wanawake walio wengi kujitokeza kushiriki katika uchaguzi mbalimbali,” alisema na kuongeza kuwa ni jambo linalosababisha idadi ndogo ya wanawake katika siasa.
Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Ulingo, Dk Avemaria Semakafu alisema lipo tatizo la rushwa ya ngono na kwamba wadau wa demokrasia wangependa kuwepo kwa uwanja sawa katika masuala ya siasa na uchaguzi.
“Suala la rushwa ya ngono tulilipendekeza kwamba liwepo kwenye sheria lakini hadi sasa halijafanyiwa kazi,” alisema.
Aidha, alisema muswada wa sheria ya vyama vya siasa haujagusa mambo ya demokrasia linganifu na kwamba sheria iwe inayovunja ubaguzi wa aina yoyote kwenye vyama vya siasa.
Kadhalika alisema hakuna sheria inayowawajibisha vyama kwenye muundo wake wa uongozi kwa kuwepo kwa sura inayozingatia jinsia kwamba iwapo mwenyekiti wa chama atakuwa mwanaume basi makamu wake awe mwanamke, hivyo suala hilo liwepo kisheria.
Kuhusu mfumo wa utoaji ruzuku alisema liangaliwe kwa vyama vyote ili kupata fedha za kuendesha shughuli zao na kuondoka mifukoni mwa watu na vyama viainishe wazi jinsi ruzuku hiyo imeweza kusaidia wanawake.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Taifa (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mary Chitanda aligusia uwakilishi wa wanawake ndani ya vyama vya siasa kwamba sheria itamke wazi katika teuzi za ndani ya chama na wanawake iwe ni zaidi ya asilimia 20.