Washauriwa kupanda uyoga una faida nyingi
MJASIRIAMALI Esther Shebe, ameishauri jamii kupanda uyoga kwa kuwa una vitamin nyingi, madini pamoja na kinga kwa baadhi ya saratani.
Shebe ambaye ni mnufaika wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), amezungumzia uyoga katika Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima Kitaifa yanayofanyika mkoani Pwani.
Amesema kupitia mfuko huo alijifunza kilimo hicho cha uyoga kilichomwezesha kuzalisha mbegu zake mwenyewe na kuziuza kwa watu mbalimbali.
“Nilipoanza kilimo hiki nilipata changamoto ya mbegu sasa nina maabara ndogo ya kuzalisha mbegu yenye uwezo wa kuzalisha chupa 500 hadi 1000.
“Chupa moja unapanda kwenye mifuko 10, ukiwa na chupa 1000 utapanda mashamba mengi. Ninapanda mbegu hizi kwa mahitaji yangu na nyingine ninaziuza ili kuongeza kipato,” amesema na kuongeza kuwa uyoga una Vitamin A, B, C, D na K pia kuna madini ya potassium na zink.
Amesema uyoga unasaidia kukinga kupata baadhi ya saratani kwa kuwa unapunguza mafuta yaliyozidi mwilini, pia ni lishe dawa inasaidia kukinga maradhi.
Kwa upande wake Ofisa Uhusino kutoka TEA, Eliafile Solla amesema mamlaka hiyo inashiriki kwenye maonesho hayo kupitia mfuko wake huo ambao unalenga kukuza na kuendeleza ujuzi katika sekta sita za kipaumbele.
Ametaja sekta hizo kuwa ni nishati, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), ujenzi, uchukuzi, kilimo, utalii na huduma za ukarimu.
“Kupitia mfuko huo mafunzo yanayotolewa yapo nje ya mfumo rasmi na juma la elimu ya watu wazima linalenga kuangalia mchango wa mafunzo yanayotolewa nje ya mfumo rasmi unavyosaidia kwenye jamii na ndio maana TEA wako hapo,” amesema.
Ameeleza wanufaika waliopata ujuzi kupitia mfuko huo wengi wameweza kujitengenezea kipato lakini pia wameweza kuwaajiri vijana wengine.
Amesema kwa miaka miaka mitano ya mfuko huo, umewezesha kunufaisha Watanzania 49,000.