WATU watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mara kwa kujaribu kukwamisha Sensa ya Watu na Makazi mjini Musoma.
Mratibu wa Sensa wa Manispaa ya Musoma, Joseph Ochora amemtaja karani wa sensa, Thomas Ndyetabura kwamba anashikiliwa na polisi tangu juzi kwa kuhesabu kaya moja tu kutwa nzima na baadaye kukutwa akiwa amelewa.
Kwa mujibu wa Ochora, karani huyo alitakiwa kuhesabu kaya kati ya 20 hadi 30 kwenye Kata ya Kwangwa, lakini baada ya matendo hayo nafasi yake ikatolewa kwa karani mwingine na kazi inaendelea.
“Changamoto nyingine imetokea Kata ya Kitaji, Barabara ya Shaban Nyumba Namba 28 ambapo kaya moja ilikataa kuhesabiwa, tumewakabidhi polisi,” amesema Ochora.
Amesema kaya hiyo ina binti aliyemtaja kwa jina moja la Leila na mama yake mzazi (hakumtaja majina) kwamba licha ya kugoma kuhesabiwa, waliwatolea maneno ya kashfa karani wa sensa.
Meneja azuia dodoso
Taarifa kutoka Arusha zinasema Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Said Mtanda amemshutumu Meneja wa Benki ya Azania tawi la Arusha, Mohamedraza Pardhan kwa kuzuia makarani wa sensa kutekeleza majukumu yao kwa watumishi wa benki hiyo.
Akizungumza na wananchi wakati akihamasisha sensa katika viwanja vya Kilombero, DC Mtanda alisema kuwa uongozi wa benki hiyo ulikwamisha zoezi hilo kwa kuwazuia makarani waliofika kwa lengo la kuchukua dodoso kwa watumishi wa benki.
“Naomba nitoe onyo kali kwa taasisi zote zilizopo wilayani Arusha kutoa ushirikiano kwenye zoezi hili na yeyote asiwe kikwazo kwa kuwa akithubutu atakiona cha mtema kuni,” alisisitiza Mtanda.
Idadi kubwa ya kaya
Na kutoka Magu, Mwanza imeandikwa makarani wa sensa wameiomba serikali kuwasaidia katika kuongeza muda wa kazi hiyo kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya watu katika kaya moja.
Hayo yamesemwa juzi na Karani wa Sensa kutoka Wilaya ya Magu, Kazimili Makungu wakati wa mahojiano na gazeti hili. Makungu alisema ukusanyaji wa taarifa za sensa zinahitaji umakini zaidi na si jambo la kukusanya taarifa hizo kwa haraka.
”Katika Wilaya ya Magu, kaya nyingi zimekuwa na watu wengi ambapo karani anaweza kutumia saa mbili. Ili kwa sisi makarani kulifanya zoezi hili kwa ufanisi na ufasaha zaidi kuna haja kubwa sana ya kuongezewa muda,” alisema Makungu.
Naye Karani wa Sensa kutoka wilaya hiyo, Deleli Lucas alisema wingi wa watu katika kaya ndio kunapelekea wao kuomba muda wa kuongeza muda wa sensa.
Ataka haraka yakuhoji
Wananchi wa Kata ya Matemanga wilayani Tunduru, wamewaomba makarani waliopewa kazi katika sensa ya watu na makazi, kuharakisha kuuliza maswali na kuchukua taarifa za kaya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema licha ya shughuli hiyo kupokelewa vizuri lakini changamoto kubwa ni makarani ambao wanatumia muda mrefu kufanya mahojiano na kujaza taarifa za kaya.
Askofu wa Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi (Kiuma) wilayani humo, Noel Mbawala alisema muda wanaotumia makarani kujaza taarifa ya kaya moja kwenye vishikwambi ni mrefu.
Hawa Athuman mkazi wa Milonde, alitaja changamoto ya shughuli hiyo kuwa ni muda mrefu unaotumika kufanya mahojiano kwenye kaya moja.
Kwa upande wake Ofisa wa sensa kutoka ofisi ya Taifa ya Takwimu anayesimamia Tarafa ya Matemanga, Nassoro Shamte alisema kwa ujumla zoezi hilo linakwenda vizuri kutokana na hamasa kubwa iliyofanywa na viongozi wa ngazi mbalimbali.
Mawasiliano kasheshe
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mangwalla amesema kuwa zoezi la sensa ya watu na makazi linaendelea vizuri wilayani hapo licha ya changamoto ya mawasiliano vijijini.
Akizungumza na mwandishi wa habari jana kwa njia ya simu, Mangwalla amesema kuwa makarani wa sensa wanaendelea kukusanya taarifa katika maeneo mbalimbali ya wilayani hapo ila wamejipanga kuhakikisha vyombo vya usafiri vipo kwa ajili ya kuwafikia wananchi katika kaya zao.
Alisema changamoto kubwa ni ukosefu wa mawasiliano ambapo vijiji 48 kati ya 65 vilivyopo wilayani Ngorongoro havina mawasiliano na kupelekea makarani wa sensa kujaza taarifa za kaya kwa kutumia vishikwambi kisha wanapomaliza kuchukua taarifa za zoezi hilo jioni wanarudi mjini eneo la Wasso kutuma taarifa kwenye mtandao.