Washindana nyimbo kusherehekea mwaka wa Kichina

Washindana nyimbo kusherehekea mwaka wa Kichina

TAASISI ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), imeadhimisha mwaka wa kichina kwa wanafunzi wa kitanzania kwa kuandaa mashindano ya kuimba nyimbo za lugha hiyo ili waielewe zaidi.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo chuoni hapo, Profesa Zhang Xaozhen amesema hayo wakati wa maadhimisho hayo yaliyofanyika UDSM.

Amesema pamoja na wanafunzi kuimba nyimbo za kichina, inawawezesha kuboresha uwezo wao wa kutumia lugha hiyo.

Advertisement

“Pia tunasheherekea sherehe hizi na watu waliopo China na kuleta furaha yetu kwa rafiki zetu Watanzania,” amesema.

Naye Mwalimu wa lugha hiyo katika taasisi hiyo UDSM, Sharif Matumbi amewataka Watanzania kusoma lugha hiyo kwani ina fursa mbalimbali ikiwemo ajira pamoja na ukalimani.

“Kunahitajika walimu wa kutosha kwenda kufundisha vyuo vikuu na kwenye sekondari, pia sasa lugha hiyo ipo kwenye mitihani ya kidato cha pili na cha nne,” amesema.

Aliongeza kuwa hivi sasa hapa nchini Wachina wapo wengi vile vile kampuni zao zipo nyingi, hivyo kunahitajika wakalimani wanaohitajika kufanya kazi na Wachina.

Naye Mwanafunzi wa mwaka wa pili chuoni hapo, Steven Mushi amesema anasoma lugha hiyo ili kuweza kuwasaidia wachina wanaokuja nchini kwenye maeneo mbalimbali, lakini pia anaongoza watalii Mlima Kilimanjaro, hivyo lugha hiyo itamrahisishia katika kazi.

Kwa upande wake mwanafunzi wa mwaka wa tatu chuoni hapo, Lulu Said amesema anasoma lugha hiyo kama fursa kwake ya kumwezesha kuwa mwalim au mkalimali, pamoja na kujifunza tamaduni mbalimbali.

Anatoa wito kwa wanafunzi kujifunza lugha hiyo kwa kuwa hivi sasa kuna fursa mbalimbali kutokana na kujua kichina.