Washukuru Awamu ya Sita kukamilisha zahanati ya miaka 13

Washukuru Awamu ya Sita kukamilisha zahanati ya miaka 13

WANANCHI wa Kijiji cha Ilanga, Kata ya Muze, Wilaya ya Sumbawanga wameishukuru serikali kwa kutoa fedha zilizosaidia kukamilisha mradi wa ujenzi wa zahanati iliyoanza kujengwa mwaka 2009.

Walitoa pongezi hizo Jumamosi wakati wa hafla ya uzinduzi wa zahanati ya kijiji hicho iliyofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Queen Sendiga ambayo serikali ilitoa Sh milioni 75 kuikamilisha.

Diwani wa Kata ya Muze ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Kalolo Ntira alisema wananchi wamefurahi kuona huduma za afya zikianza kutolewa baada ya ujenzi ulioanza miaka 13 iliyopita kwa nguvu za wananchi kukamilika.

Advertisement

“Kata ya Muze ina zaidi ya watu 32,000 ikiwa haina kituo cha afya, hivyo leo kuanza kutumika wa zahanati ya Kijiji cha Ilanga ni mafanikio makubwa. Tunaishukuru serikali,” alisema Kalolo.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Lightness Msemo alisema zahanati hiyo itahudumia wananchi 4,263 wa Kijiji cha Ilanga na wananchi 3,886 wa Kijiji cha Mlazi Asilia.

Akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara, Sendiga aliwapongeza wananchi wa Kijiji cha Ilanga kwa kazi nzuri ya kuanzisha mradi huo kwa kuchangia nguvu na fedha.

Sendiga alisema mradi huo ambao umegharimu Sh milioni 150, ni mkombozi kwa wananchi kupata huduma bora za afya karibu.

 

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *