Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi, wameishukuru serikali kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka Vikonge hadi Uvinza mkoani Kigoma kwa kiwango cha lami.
Wakizungumza mbele ya msafara wa Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu aliyeambatana na viongozi wengine walipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa barabara ya Vikonge – Luhafwe (Km 25), wamesema walilazimika kukatiza maporini kufuata huduma za afya jambo lililosababisha vifo kwa baadhi ya mama wajawazito.
“Tulipata shida sana, unakuta mama mjamzito anatoka mbali wanapopatwa na uchungu mtu anazalia njiani, ” amesema Devotha Titto mkazi wa Kijiji cha Vikonge.
Amesema mbali na kuwarahisishia usafiri, lakini pia ana imani hata kiwango cha nauli kitakuwa chini ikiwemo ufupi wa safari kutoka Mpanda hadi Kigoma, kwani kwa sasa wanatumia hadi saa sita kufika mkoani Kigoma.
Diwani wa Kata ya Tongwe, Frank Kibigasi amesema kukamilika kwa barabara hiyo ya Mpanda – Kigoma itafungua fursa kwa wakazi wa Tanganyika na Katavi kwa ujumla kufanya biashara Kigoma na nchi jirani za DRC, Rwanda na Burundi kwa kuuza mazao yao kwa kuwa mkoa wa Katavi ni wa kilimo.
“Tunamshukuru sana Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi alizoshusha kwenye miradi mbalimbali hasa kwenye hii barabara itakuja kuwa mkombozi na itakuja kuinua uchumi wetu,” amesema.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji mradi huo, Kaimu Meneja Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Katavi, Mhandisi Emily Zengo amesema barabara hiyo inajengwa kwa fedha za ndani kwa gharama ya sh. bilioni 35.638.
Amesema, kazi inayofanyika ni ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, kukata sehemu ambazo milima iko juu sana, ujenzi wa daraja kubwa Mnyamasi lenye urefu wa mita 61.8 na kina cha mita 5, ambalo litakuwa suluhisho eneo hilo kwa kuwa mvua zinaponyesha maji yanapita juu ya barabara.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu amesema ziara hiyo ni kwa ajili ya kuadhimisha miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambapo amemuahidi Rais Dk Samia Suluhu Hassan kusimamia miradi yote na fedha zote kwa ufanisi zaidi, ili wananchi waweze kupata thamani ya fedha zinazotolewa na serikali.