WASICHANA 6,685 wenye umri kati ya miaka 13 na 21 waliokatisha masomo ya sekondari kwa sababu mbalimbali ukiwemo ujauzito wamejisajili kuendelea na masomo kwa njia mbadala. Wanaendelea na masomo kupitia Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP- AEP).
Mradi huo unatekelezwa na taasisi iliyopo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa ufadhili wa Benki Dunia. Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Dk Michael Ng’umbi alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa Baraza la 13 Wafanyakazi wa Taasisi hiyo mjini Morogoro.
Dk Ng’umbi alisema mradi huo unaotekelezwa na taasisi hiyo ulianza mwaka jana na ulisajili wasichana 3,333 wanaoendelea na masomo kwenye vituo vya taasisi hiyo. Alisema kwa mwaka wa masomo wa 2023 na hadi kufikia Februari mwishoni, wasichana 3,352 tayari wamejisajili kuendelea na masomo yao.
Dk Ng’umbi alisema mradi huo unalenga kunufaisha wasichana 12,000 nchini ambapo kila mwaka utasajili wanafunzi 3,000 kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2022 hadi 2026.
Alisema mradi huo unalenga kuwapatia elimu ya sekondari bila malipo wasichana waliokatisha masomo ya elimu ya sekondari. Dk Ng’umbi alisema katika kuendesha na kusimamia elimu mbadala nje ya mfumo wa shule, taasisi imeandaa mitaala na kuendesha programu kwa kutumia mfumo huria na masafa.
Alisema lengo ni kuwafikia walengwa walio wengi zaidi nchini ambazo kwa pamoja hutolewa kwa elimu ya sekondari kwa njia mbadala. Pia aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kugharamia ujenzi wa hosteli na kutoa chakula kwa wasichana hao ili kiwe kichocheo cha kuhudhuria masomo hayo ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.
Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Michael John aliagiza taasisi hiyo kuhakikisha inasimamia vema miradi hiyo. John alisema hatua hiyo ni kwa ajili ya kufikia malengo yote yaliyowekwa katika miradi ukiwemo wa SEQUIP.
Aliagiza taasisi hiyo kuanzisha kozi ambazo zinaendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia pamoja na utandawazi ambazo zinakidhi mahitaji ya soko la ajira na ushindani katika uchumi wa sasa.