Wasichana waahidiwa mazingira mazuri masomo ya sayansi

DSM; Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imesema itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kuongeza ushiriki wa wasichana katika fani za sayansi na teknolojia, ili kuongeza wataalamu wengi zaidi wa kike katika soko la ajira nchini.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Kennedy Hosea, wakati alipomwakilisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo katika ufunguzi wa kozi ya Foundation inayotolewa katika chuo Kikuu huria cha Tanzania kwa wasichana 140.

Wasichana hao ni waliomaliza kidato cha sita na  kupata changamoto mbalimbali zilizowafanya kushindwa kuendelea na elimu ya chuo Kikuu kwa upande wa masomo ya sayansi kwa ufadhili wa Mradi wa HEET, ambao uko chini ya Benki ya Dunia na Wizara ya Elimu.

Mkurugenzi huyo amesema lengo la serikali katika programu hiyo ni kuongeza kwa wingi watalaamu katika fani hizo za sayansi, hususani watoto wa kike na kuwataka wasichana hao kutumia fursa hiyo waliyoipata kuhakikisha wanatimza malengo yao kupitia kozi hiyo, ili waweze kuingia vyuoni na baadae waweze kulisaidia Taifa kupitia taaluma waliyopata vyuoni.

Awali akizungumza katika ufunguzi huo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Profesa Elifas Bisanda pamoja na mambo mengi aliweka msisitizo kwa wanafunzi hao kuhakikisha wanasoma na kufikia ufaulu utakaowawezesha kupata elimu ya vyuo vikuu.

Habari Zifananazo

Back to top button