Wasichana wanatamani kutimiza ndoto zao lakini…!

NOVEMBA 24 mwaka 2021, historia iliandikwa hapa nchini kufuatia uamuzi wa serikali kuruhusu kurejea shuleni wanafunzi waliokatiza masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito.

Uamuzi huo uliambatana na waraka uliotoa mwongozo wa wanafunzi hao walioacha masomo kurejea shuleni na kuendelea na masomo.

Hata hivyo, miaka miwili baada ya uamuzi huu kufanyika, bado kuna kusuasua kwa wanafunzi hasa waliopata ujauzito kurejea shuleni kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mazingira kutokuwa rafiki kwao.

Taasisi ya Msichana Initiative iliyotombelea Wilaya ya Kongwa na Nzega kuangalia utekelezwaji wa sera ya kurudi shule kwa wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu ya ujauzito, umebaini kuwa wasichana nane kati ya 10 waliopata ujauzito sawa na asilimia 85 wanatamani kurudi shule.

Asilimia 15 iliyosalia wanahitaji jitihada zaidi kufanyika katika kutengenezamazingira wezeshi kwao na kwa watoto wao, ili waweze kusoma bila kukutana na vikwazo ikiwemo msongo wa mawazo.

Hilo linawafanya wengi wachague kutafuta maarifa nje ya mfumo rasmi wa elimu kwa kile wanachoona kurudi shuleni kutawapotezea muda na baadala yake ni heri wapate mafunzo yatakayowawezesha kujiajiri ndani ya muda mfupi.

Mfano wa hilo unaonekana katika Wilaya ya Kongwa, ambapo wasichana 15 waliohojiwa wameonesha wako tayari kurudi shule, ingawa asilimia 50 kati yao wanahitaji zaidi kurejea katika mfumo usio rasmi, ikiwemo mafunzo ya ufundi au madarasa ya ujasiriamali yatakayowasaidia kujifunza jinsi ya kutengeneza fedha ili wawasaidie watoto wao.

Wilayani Utafiti huo umeonesha kuwa kwa kiasi fulani kuna mazingira wezeshi kwa wasichana wanaorejea shuleni, ingawa bado kuna changamoto ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi.

Baadhi ya wasichana waliohojiwa kwenye utafiti huo wameeleza kukosekana kwa mabweni kwa wanafunzi wanaoishi mbali na shule, kukosekana kwa chakula, kukosekana kwa walimu wa saikolojia ambao wanaweza kuwasaidia kuwajenga kisaikolojia baada ya kurejea shule ni miongoni mwa vikwazo.

Miongoni mwa wasichana waliopata vikwazo ni Habiba Nemelegani (17) mwanafunzi wa kidato cha pili na mama wa mtoto wa miezi sita ni miongoni mwa maelfu ya wasichana ambao ndoto zao zimefufuliwa  kufuatia uamuzi wa serikali kuruhusu mabinti waliokatisha masomo kwasababu ya ujauzito kurejea shuleni baada ya kujifungua.

‘’Nilikata tamaa, nikiangalia familia yangu na jinsi baba yangu alivyokuwa mkali nikaona nimetenda kosa kubwa ambalo adhabu yake itagharimu maisha yangu yote.

“Nashukuru Mungu alikuwa upande wangu, Serikali ikatoa nafasi nyingine kwangu kurejea shuleni na wazazi wangu wakawa tayari kunisaidia kwenye malezi ya mtoto ili isiwe kikwazo kwenye masomo yangu, ‘’ anasema

Naye Baba mzazi wa Habiba, Kibwana Nemelegani anasema taarifa ya ujauzito wa mtoto wao ilifedhehesha familia lakini hakuwa na la kufanya zaidi ya kuhakikisha mtoto wake anarudi shuleni.

Kwa upande wake mwalimu wa nidhamu katika sekondari anayosoma Habiba, Chananja anasema taarifa za ujauzito wa mwanafunzi huyo ziliwapa wakati mgumu walimu kwa sababu alikuwa miongoni mwa wanafunzi wanaotegemewa kutokana na uwezo wake.

“Ni mtoto ambaye alikuwa vizuri sana kitaaluma hivyo tulipopata taarifa kwamba ana ujauzito kiukweli tulisikitika, tunachokifanya ni kumjenga kisaikolojia ili akili yake yote aiweke kwenye masomo,” anasema.

Hatua za kuchukua

Wadau wa elimu wameishauri Serikali kushirikiana na sekta binafsi kutatua changamoto zinazowavuta nyuma wasichana waliopewa fursa ya kurejea shuleni baada ya kukatisha masomo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo ujauzito.

Anasema jambo jingine analoshauri ni kuwepo maeneo maalumu kwa ajili ya watoto wa wanafunzi waliorejea masomoni, kwani ni ngumu mwanafunzi kuingia darasani huku hajui hatma ya mwanawe.

“Mfano Kenya baadhi ya shule za umma zimetengeneza mazingira wanafunzi wa namna hiyo wanakwenda na watoto, hivyo serikali iangalie hilo kwa sababu ni kweli hao wanafunzi hawawezi kuwatelekeza watoto wao wakawaacha bila watu wa kuwaangalia,’’ anasema Ndossa.

Umuhimu wa kufanya hivyo unaelezwa pia na Dk Avemaria Semakafu  ambaye anasema haki ya binti inapoangaliwa kwenye kusoma ni lazima kuangalia pia haki ya mtoto aliyezaliwa.

“Changamoto kwa wanafunzi wanaokatisha masomo wanatoka katika familia fukara unapomwambia arejee bila kumpa njia ya kurejea yule anayeachwa nyumbani itakuwa nini.

“Unaposema huyu arudi shule anamwachia nani mtoto, sasa mwanamke akishajifungua kipaumbele chake ni mtoto na si kitu kingine sasa amuone mtoto wake kule hana uwezo wa kumnunulia maziwa,unamwambia mjoo huku.

“Tunaomba Serikali ichukue hatua kwa kuweka mazingira rafiki na salama kwa wasichana wanaorejea shuleni lakini pia wafanyie kazi baadhi ya mapungufu yaliyopo kwenye mwongozo wa kurejea shule,”anasema Dk Avemaria

Habari Zifananazo

2 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button