Wasimamizi wa uchaguzi wafundwa

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo na kata kufanyakazi kwa weledi kwa kuzingatia katiba ya nchi na maelekezo ya tume hiyo.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele alisema hayo Agosti 8,2023 mjini Morogoro wakati akifungua mafunzo ya watendaji wa uchaguzi mdogo wa mbunge na madiwani wa kata yenye lengo la kukumbushana mambo muhimu ya usimamizi, uratibu na uendeshaji wa uchaguzi.

Mwambegele alisema uchaguzi mdogo wa mbunge unatarajiwa kufanyika jimbo la Mbarali pamoja na madiwani katika kata sita Tanzania Bara.

“Mnatakiwa kutambua kuwa mmeaminiwa na kuteuliwa kwa sababu mnao uwezo wa kufanya kazi hii, mnalotakiwa kuzingatia ni kujiamini na kufanya kazi kwa weledi, kwa kuzingatia katiba ya nchi, sheria na kanuni za uchaguzi na maelekezo yanayotolewa na Tume.” Alisema Mwambegele

Mwenyekiti wa NEC , Jaji  Mwambegele aliwasisitiza kufanya utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema, kuhakikisha wanaajiri  watendaji wa vituo wenye weledi, kuhakiki vifaa vya uchaguzi wanavyopokea kutoka tume pamoja wakuu wa vituo kuhakikisha wanapata vifaa vyote vinavyohitajika katika uchaguzi kwa wakati.

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhan Kailima alitaja uchaguzi mdogo huo utafanyika  Septemba 19, 2023 katika Jimbo la Mbarali.

Habari Zifananazo

Back to top button