TANGA: Watu wasiojulikana wameiba magunia mawili ya misumari katika mradi wa hospitali ya Wilaya ya Pangani
Mkuu wa Wilaya ya Pangani Zainab Abdallah ameweka bayana hilo wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Chama Cha mapinduzi Mkoa wa Tanga Rajab Abdurahman aliyefanya ziara ya kushtukiza hospitalini hapo.
Amesema kuwa baada ya kubaini wizi huo ameuagiza uongozi wa hospitali hiyo kuweza kuripoti kwenye vyombo husika ili hatua za kisheria ziweze kufuatwa.
“Tayari taarifa imeweza kutolewa na taratibu nyingine zinafuatwa kwani mradi huu ni muhimu kwa wananchi wa Wilaya hii”amesema.
Hata hivyo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Rajabu Abdurahman amemuagiza Mkuu wa kituo cha Polisi Wilaya ya Pangani(OCD) kuwachukulia hatua za kisheria wabadhilifu wa vifaa vya ujenzi wa Hospitali ya wilaya hiyo.
Mbali ya agizo hilo pia amemuomba Mkuu wa wilaya hiyo na kamati ya ulinzi na usalama kutembelea mara kwa mara hospitailini hapo ili kutokuwapa nafasi watu wanaohujumu mradi huo ambao Serikali imetenga Sh milioni 900 kwa ajili ya maboresho na ujenzi wa majengo mapya.