Wasioolewa wakacha uzazi wa mpango

IDADI ya wanawake wasioolewa wanaotumia njia wa uzazi wa mpango imepungia kutoka asilimia 46 kwa Utafiti wa mwaka 2015/16 hadi asilimia 36 kwa Utafiti wa mwaka 2022.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alisema hayo  wakati wa uzinduzi wa matokeo muhimu ya utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya malaria Tanzania wa mwaka 2022.

Alisema kuwa matokeo yameonesha miongoni mwa wanawake walioolewa, matumizi ya njia yoyote ya kisasa ya uzazi wa mpango ni takriban sawa na iliyoripotiwa katika utafiti wa mwaka 2015/16.

Alisema kuwa utafiti umeonesha asilimia 38 ya wanawake walioolewa kwa sasa wanatumia njia yoyote ya uzazi wa mpango, ikijumuisha asilimia 31 wanaotumia njia yoyote ya kisasa na asilimia saba ya wanawake wanatumia njia ya asili ya uzazi wa mpango.

Hata hivyo, wanawake wasioolewa lakini wanashiriki tendo la kujamiiana, matumizi ya njia yoyote ya kisasa yamepungua kutoka asilimia 46 kwa Utafiti wa mwaka 2015/16 hadi asilimia 36 kwa Utafiti wa mwaka 2022.

Aidha alisema kiwango cha vifo vya watoto wachanga kabla ya kutimiza mwaka mmoja ni vifo 33 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa hai kwa Mwaka 2022 ukilinganisha na vifo 43 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa hai mwaka 2015/2016. Kiwango cha vifo vya watoto wachanga kabla ya kutimiza mwezi mmoja ni vifo 24 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa hali.

Matokeo yanaonesha pia kuwa, asilimia ya wanawake waliohudhuria vituo vya kutolea huduma wakati wa ujauzito mara nne au zaidi ni kubwa katika Mkoa wa Dar es Salaam (asilimia 90.2), ikifuatiwa na Mjini Magharibi (asilimia 86.5),Kusini Unguja (asilimia 84.1) na Mtwara (asilimia 82.5).

Mikoa ambayo ipo chini kwa mahudhurio ya vituo vya kutolea huduma wakati wa ujauzito ni Simiyu(asilimia 36.0), Katavi (asilimia 41.6) na Shinyanga (asilimia 44.9).

Habari Zifananazo

Back to top button