Wasiovaa hijab kukamatwa Iran

MAMLAKA nchini Iran imetangaza kampeni mpya ya kuwakamata wanawake wasiovaa hijabu, huku polisi wa maadili wakielekezwa kuanza doria kutekeleza sheria za lazima za hijab.

Saeid Montazeralmahdi, msemaji wa kikosi cha kutekeleza sheria cha Iran, alithibitisha Jumapili kwamba doria za polisi sasa zinafanya kazi kwa miguu na kwa magari ili kukabiliana na watu ambao mavazi yao hayaonekani kuwa yanafaa katika Jamhuri ya Kiislamu.

Montazeralmahdi alisema polisi wanatarajia kila mtu kufuata kanuni za mavazi zinazokubalika ili maafisa wawe na muda zaidi wa kushughulikia misheni nyingine muhimu za polisi.

Advertisement

“Maafisa hao wana jukumu la kuwaonya wanawake na wakati mwingine wanaume kuwarekebisha jinsi wanavyovaa. Hii inaweza kuanzia kuwaamuru wanawake kurekebisha hijabu.” Alisema Montazeralmahdi.

Wanawake wanaofikiriwa kukiuka sheria wanaweza kukamatwa na kupelekwa kwenye kile kinachoitwa vituo vya elimu upya vinavyoendeshwa na polisi kwa ajili ya kupatiwa elimu zaidi ya namna gani wanapaswa kujistiri.

Taarifa hizo zinakuja miezi 10 baada ya Mahsa Amini, 22, kufariki akiwa mikononi mwa polisi baada ya kuzuiliwa kwa madai ya ukiukaji wa kanuni za mavazi.

Kifo chake kilisababisha maandamano makubwa nchini kote ambayo yalidumu kwa miezi kadhaa ambapo polisi wa maadili walishindwa kujitokeza mitaani.

Baada ya maandamano hayo, viongozi wa Iran kwa kiasi kikubwa walijiepusha na mbinu za mabishano za kutekeleza sheria za lazima za hijab ambazo ziliwekwa muda mfupi baada ya mapinduzi ya Kiislamu ya 1979 nchini humo. Njia hiyo inaonekana kuwa inabadilika hatua kwa hatua.