Wasomi watoa ushauri marekebisho tozo

SERIKALI imeshauriwa kuzingatia masuala kadhaa inaporekebisha tozo za miamala ya kielektroniki ukiwamo ubunifu, wataalamu wa uchumi, kupanua wigo wa walipa kodi na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Hivi karibuni, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiliiagiza serikali izingatie maoni ya wananchi kuhusu tozo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba ameahidi muda si mrefu watatoa majibu katika hilo. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Mushi alisema serikali inapaswa kuongeza ubunifu ili kuongeza wigo wa mapato.

“Kiukweli tozo zinakuwa mzigo kwa sasa kwa sababu ya ukosefu wa ubunifu kwani zinatozwa eneo lilelile bila kupanua wigo,” alisema Profesa Mushi. Aliongeza: “Kuna watu ambao hawalipi kodi kutokana na uchumi na kipato chao.

Kwa mfano, kuna gereji kila mahali, vituo vya mafuta vinajengwa kila kona vinasimamiwa ipasavyo kulipa kodi?” Alisema serikali isipokuwa makini watu watazikimbia benki na hata huduma za kibenki za simu na kuweka fedha kwenye magodoro au kutumia njia za kawaida kutumiana fedha.

“Serikali imeonesha kuwa ni sikivu na imesikia kilio cha wananchi chini ya Rais Samia. Lakini ni muhimu kuhakikisha kila mtu analipa kodi. Tukipanua wigo wa kodi kila mtu atalipa zitapatikana fedha nyingi kuliko kutoza kodi watu walewale,” alisisitiza.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar Idara ya Uchumi, Profesa Haji Semboja aliiomba serikali izingatie ubunifu na itafute vyanzo vingine vya mapato badala ya kuweka nguvu kubwa kwenye tozo za miamala.

Profesa Semboja alisema tozo hailengi kuingizia serikali mapato bali kusaidia eneo maalumu inakotozwa ikiwemo kudhibiti matumizi ya jambo au kitu fulani.

“Kama Seychelles ni nchi ambayo pato lake la taifa ni kubwa kuliko Tanzania, dola za Marekani 1,200 inatumia tu utalii kupata mapato. Botswana yenyewe pato lake la taifa ni dola za Marekani 2,500 yenyewe imeweka mkakati mwekezaji yeyote anawekeza nchini humo, lazima serikali iwe na asilimia 50 ya hisa. Mbinu ziko nyingi watumie tu wachumi watafanikiwa,” alisisitiza.

Mchambuzi wa Masuala ya Siasa, Uchumi na Diplomasia, Abbas Mwalimu alisema kuna haja ya ubunifu wa maeneo ya kuingizia kipato serikali badala ya kujikita katika eneo moja la kodi na tozo.

“Naomba ianze kuangalia kiwango cha kodi, lakini katika eneo la progressive tax. Kodi hiyo inayoendelea imewekwa kwenye eneo moja tu la mshahara kwa watumishi. Mamlaka husika kama vile Wizara ya Fedha na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zinapaswa kupanua wigo zaidi za kutoza kodi hii kwa watu wengi zaidi na si kuelemea eneo moja,” alisema Mwalimu.

Aliiomba serikali izingatia matumizi ya tehama katika kukusanya kodi ili kuongeza wigo wa walipa kodi. Alisema sensa iliyofanyika mwaka huu inaweza kutumika kutambua makundi ya sekta zisizo rasmi yanayostahili kutozwa kodi wakiwamo bodaboda, mama ntilie, mafundi gereji na hata madereva na makonda wa daladala.

“Mama ntilie na wafanyabiashara wengine wadogo wanaweza kupewa mashine za EFDs kwa mkopo mdogo na kutoa risiti kila wanapouza bidhaa. Nchi kama Marekani au Uturuki hata ukila kwa mama ntilie unapewa risiti, hii itaweza kila mtu kulipa kodi kulingana na kipato chake,” alisema Mwalimu.

Habari Zifananazo

Back to top button