DAR ES SALAAM: Mfuko wa hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma ‘PSSSF’ umeeleza kuwa unaendelea na uwekezaji ili kutoa huduma zitakazoondoa kabisa changamoto katika utoaji huduma kwa wanufaika wa Mfuko huo.
–
Hayo yamesemwa leo Agosti 31, 2023 katika Mkutano wa Mfuko huo na Wahariri pamoja na Waandishi wa habari ikiwa ni tekelezo la agizo la Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu kuzitaka taasisi na Mashirika ya Umma kukutana na Jukwaa hilo.
–
Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA Hosea Kashimba amesema ndani ya kipindi cha miaka mitano ya mfuko huo kwa kiwango kikubwa wameshughulikia changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili Wastaafu kutoka maeneo mbalimbali nchini.
–
“Tumefanikiwa katika kulipa bila kukosa na kwa wakati pensheni ya kila mwezi, Wastani wa shilingi bilioni 67 hulipwa kila ifikapo tarehe 25 ya mwezi husika, hili ni ongezeko la asilimia 100 ukilinganisha na kiasi cha shilingi bilioni 34 zilizokuwa zikitolewa hapo awali kila mwezi.” amesema kashimba
–
Aidha ameongeza kuwa thamani ya mfuko huo imeongezeka kwa asilimia 27.76 kutoka shilingi Trilioni 5.83 hadi trilioni 8.07 na kupunguza gharama za uendeshaji.
–
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri wa vyombo vya habari Tanzania Deodatus Balile amesema Taasisi na Mashirika ya Umma ni vyema yakatumia vyombo vya Habari kuujulisha Umma utendaji kazi wake.
“Taasisi hizi zinafanya mambo makubwa sana lakini wananchi hawajui yale yanayofanyika, kwahiyo ni vyema tukaendelea kushirikiana ili kulijenga taifa moja” amesema Balile.
–
PSSSF inakuwa ni Taasisi ya nane kukutana na Jukwaa hilo ambapo lengo kuu la makutano hayo ni kuboresha utendaji kazi wa Taasisi na Mashirika ya Umma.
Comments are closed.