Kikundi cha wastaafu kutoka kijiji cha Kididumo, mkoani Morogoro wametembelea Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni pamoja na Kijiji cha Makumbusho na kuwataka wastaafu kutumia muda wao vizuri kutembelea vivutio mbalimbali nchini.
Mlezi wa Kikundi hicho cha Kididimo Upendo Women Group and Familiy, Dk Peter Mtakwa, amesema kuwa wastaafu wanaweza kutumia muda walionao kufanya utalii wa ndani, ikiwa ni pamoja na kutembelea vituo vya makumbusho ya Taifa.
“Natoa wito kwa wastaafu wenzangu kutumia fursa ya muda walionao na rasilimali walizonazo, kufanya utalii wa ndani, kwa lengo la kuburudika na kujifunza, wasingoje mpaka waishiwe nguvu kabisa, amesema Dk Mtakwa, ambaye alikuwa mwalimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine.
Amesema kuwa katika Jiji la Dar es Salaam, kumekuwa na mabadiliko makubwa na vitu vingi vipya, ambavyo havikuwepo miaka ya nyuma na wananchi wangeweza kuviona na kujifunza ikiwemo, daraja la Kigamboni, Daraja la Tanzanite, majengo, maonesho mapya, Makumbusho ya Taifa na vingine vingi.
Naye Mwenyekiti wa kikundi hicho, Dyness Kilonzo, amesema wamekuwa wakitembelea maeneo mbalimbali kwa ajili ya kufanya utalii, lakini hawakuwahi kutembelea Makumbusho na kwamba walikuwa hawajui kuwa kuna vitu vingi vya kujifunza.
“Wajukuu wamekuwa wakituuliza maswali kuhusiana na historia ya Tanzania na vitu mbalimbali vinavyopatikana Makumbusho, hatukuwa na majibu sahihi, lakini sasa tunayo majibu ya kuwaambia wajukuu zetu,” amesema Kilonzo.
Amesema wamefurahishwa sana na vitu vingi vinavyopatikana Makumbusho ya Taifa na kuahidi kutoa elimu kwa wengine kutembelea Makumbusho za Taifa, ambapo watajifunza vitu vingi.
Naye Ofisa Uhusiano Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Joyce Mkinga, aliwakaribisha wastaafu hao wapatao 30 na kuwaomba kuendelea kutoa elimu kwa wastaafu wengine, kutembelea vituo vya makumbusho na malikale, ambavyo viko maeneo mbalimbali ya Tanzania.