Wastaafu waomba kutatuliwa changamoto

ZAIDI ya wastaafu1200 wamekutana na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Halima Dendego na kuiomba serikali izifanyie kazi changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na mafao madogo na huduma duni za afya.

Kwa kupitia risala yao iliyosomwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wastaafu Tanzania Mkoa wa Iringa, John Sichone walitaja changamoto nyingine inayopaswa kuangaliwa na serikali na kufanyiwa mabadiliko kuwa ni matumizi ya kikotoo ili kuondoa athari zitakazodumu kwa kipindi kirefu kwa wastaafu.

“Kikotoo kipya kilichoanza kutumika Julai 2023 kimeacha shida vilio na kuleta sonona kwa wastaafu. Tunaomba serikali iyachukue maoni yetu kuhusu kikotoo hicho na kuyafanyia kazi,” alisema.

Advertisement

Kihongozi huyo alisema baadhi ya wastaafu hali zao za maisha zimeendelea kuwa duni kwasababu hakuna ongezeko la mafao kwa muda mrefu hali inayo sababishwa na ufuatiliaji hafifu wa serikali.

Kuhusu huduma za afya kwa wazee alisema pamoja na kwamba wanatibiwa kwa msamaha wa serikali mara nyingi wamekuwa wakikosa huduma iliyo bora.

“Suala la matibabu kwa wale ambao tuna kadi za bima ya afya sio tatizo kubwa sana lakini zile huduma zinazopatikana kwa kadi ya kupewa hilo kwa kweli limekuwa gumu kutekelezwa,” alisema.

Akiwajibu wastaafu hao, Mkuu wa Mkoa alisema serikali inataka kuona wastaafu wakiishi kwa amani na kuongeza siku zao duniani hivyo kwa kuzingatia uchumi wa nchi, mazingira na manufaa kwa pande zote mbili changamoto zao zitafanyiwa kazi.

“Changamoto zenu nimezichukua, zile tunazoweza kuzifanyia kazi kwa ngazi ya mkoa zitashughulikiwa na zile zinazohitaji mamlaka za juu basi tutaziwasilisha huko,” alisema.

Dendego alizungumzia pia utekelezaji wa Ilani ya CCM mkoani kwake akisema; “Mkoa wa Iringa umekuwa ukipokea wastani wa Sh Bilioni 230 kwa mwaka kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za maendeleo.”

Alisema maboresho yanayofanywa na serikali ya Dk Samia Suluhu Hassan katika sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo afya, maji, umeme, barabara na huduma nyingine za kijamii ni muhumu kwa ustawi wa jamii wakiwemo wastaafu hao.

Katika hatua nyingine Dendego amewaagiza watendaji mbalimbali mkoani humo kuhakikisha wanatenga maeneo maalumu kwa ajili ya kuwahudumia wazee na wastaafu .

“Maeneo hayo Mkoani kwetu yapo lakini mengi yapo kama picha; madirisha ya kuhudumia wazee yapo na dawa zipo lakini wahudumu hawapo. Kuanzia leo hilo nisilisikie, ninasema nikijiamini kwasababu huduma za dawa muhimu kwa sasa mkoani Iringa tumefikia asilimia 92, kwahiyo hakuna sababu ya wezetu waliotuhudumia na wakaijenga Tanzania wakaendelea kunyanyasika wakija maofisini mwetu, hii sio sawa,” alisema.

Sambamba na hayo mkuu wa mkoa wa Iringa ameahidi kutoa ofisi kwajili ya kuendeshea shuguli za wastaafu wa mkoa wa Iringa.

Naye Mratibu wa Umoja wa wa Wastaafu Tanzania Ezekiel Oluochi alitoa ombi kwa mkuu wa mkoa wa Iringa kuwapatia kiwanja ili kuwawezesha kujenga ofisi ya Umoja wa Wastaafu Mkoani Iringa.

/* */