Wataalamu watumie takwimu kuboresha huduma za afya

WITO umetolewa kwa wataalam wa afya kuzingatia matokeo ya utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya Malaria wa mwaka 2022 katika kuandaa mikakati na mipango ya kuboresha sekta ya afya.

Wito huo umetolewa na Meneja Takwimu za Jamii Kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Silvia Meku mjini Iringa wakati ofisi hiyo ikitoa matokeo ya utafiti huo kwa wadau wa kanda ya nyanda za juu kusini.

Akitoa taarifa ya utafiti huo kwa wadau wa sekta hiyo waliokutana katika ukumbi wa Chuo cha Afya mjini Iringa, Meku alisema matokeo ya utafiti huo yametoa picha ya hali halisi ya huduma za afya ya uzazi na mtoto katika mikoa ya nyanda za juu kusini na yatawasaidia wataalam kuweka mikakati inayoendana na hali halisi ya huduma zilivyo hivi sasa.

Akifungua mkutano huo, mwakilishi wa kKatibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Dk Chrisantus Ngongi alisema mikoa ya nyanda za juu kusini inapaswa kuwekeza nguvu kubwa katika kukabiliana na tatizo la udumavu kutokana na matokeo ya utafiti kuonyesha kanda hiyo inaongoza nchini kwa kuwa na asilimia 46 ya kiwango cha udumavu.

Kwa kugawiwa kwa matokeo ya utafiti huo kwa mikoa ya nyanda za juu kusini alisema, itasaidia wataam kupanga mipango thabiti na kupunguza changamoto zinazoikabili kanda hiyo ukiwemo udumavu huo na kusaidia kupunguza zaidi vifo vya uzazi na watoto.

Mwailishi wa Wizara ya Afya, David Edward amepongeza juhudi za serikali ya awamu ya sita katika kuimarisha huduma za afya na kupunguza idadi ya vifo vya uzazi akisema kwa sasa wanawake wengi wanajifungua katika vituo vya afya badala ya majumbani.

Naye mtaalam wa lishe kutoka mkoa wa Iringa, Bertha Mwakabage amesema mkoa wa Iringa ambao unachangamoto kubwa ya lishe umejipanga kutumia matokeo ya utafiti huo katika kutoa elimu na kuandaa mikakati mbalimbali ya kuimarisha lishe katika wilaya za mkoa huo

“Tumejipanga kutumia matokeo ya utafiti huu kuelimisha wananchi kuhusu lishe hasa uzalishaji na matumizi ya mazao ya protini ili kuimarisha lishe,” alisema.

Semina hiyo ya siku mbili inawakutanisha wataalam mbalimbali wa ngazi ya wilaya na mikoa wakiwemo waganga wakuu, waratibu wa malaria, maafisa lishe, wauguzi wakuu na waratibu wa UKIMWI kutoka mikoa ya Iringa na Ruvuma.

Habari Zifananazo

Back to top button